Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi Zanzibar kimesema hakitowavumilia baadhi ya watu wachache wanaotumia hati bandia kupora mali za chama hicho kwa makusudi.
Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar katika mwendelezo wa ziara ya kuhakiki na kukagua mali za Chama na Jumuiya zake huko katika jengo la mradi wa UVCCM Zanzibar uliopo darajani Unguja.
Vuai alieleza kwamba CCM itawachulilia hatua za kisheria baadhi ya watu watakaobainika kupora mali zake, kwani watakuwa sio watu wema wanaotaka chama hicho kisonge mbele kimaendeleo.
Alisema CCM italinda mali zake kwa gharama yoyote ili kuhakikisha hazihujumiwi na baadhi ya watu wachache wasiokitakia mema chama hicho.
Alieleza kwamba chama hicho kitapambana na watu wanaohujumu mali za chama hata kama watakuwa wanatoka ndani ya chama hicho.
Aliwataka viongozi wa CCM na jumuiya zake kuhakikisha wanalinda na kusimamia vizuri mali za chama hicho ili zibakie kuwa katika ulinzi wa kudumu.
Vuai alisema bila ya kuweka mikakati endelevu ya kulinda rasilimali za chama hicho zitapotea kidogo kidogo na kumalizika kabisa na kumilikiwa na watu wachache wasiopenda kuona CCM inapata maendeleo.
“ Mali hizi hazikubatikana kirahisi kama ambavyo baadhi ya watu wanaojimilikisha rasilimali zetu kinyume na sheria wanavyodhani, mimi nawambia waache tabia hiyo na ambao tayari wameshachukua wazirejeshe mapema vinginevyo watapambana na mkono wa sheria.’, alisema Vuai.
Naye Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrissa alisema mradi huo unaosimamiwa na umoja huo kwa kushirikiana na mwekezaji mzalendo wa Kampuni ya Mishely Co. LTD unaendelea vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto za kiutendaji zinazokwamisha mradi huo kutokamilika kwa wakati.
Alisema endapo Chama na jumuiya kwa kushirikiana na mwekezaji huyo watakaa pamoja kwa kujadiliana ili wapate maamuzi ya pamoja yatakayosaidia kutatua changamoto hizo kwa haraka.
Idrissa alikiahidi chama hicho kuendelea kulinda mali za umoja huo ili zisiingie katika mikono ya watu wenye tabia za kitapeli.
Wakati huo huo alitembelea eneo la chama hicho lililopo makontena Vikokotoni Zanzibar , alisema CCM inakusudia kuanzisha mradi wa kujenga majengo ya kisasa yatakayojumuisha maduka na ofisi ili kuwatengenezea mazingira mazuri wafanyabiasha wa maeneo hayo.
Aliwasihi wafanyabiashara wa eneo hilo kutoa ushirikiano wakati chama hicho kitakapohitaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa.
Alisema lengo la CCM ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha Zanzibar inakuwa na majengo ya kisasa na yenye hadhi yatakayowavutia wafanyabiashara wakubwa kuwekeza katika eneo hilo .
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema muonekano wa eneo hilo linalofanyiwa biashara kwa sasa umepitwa na wakati unahitaji uimarishwaji wa miundo mbinu unaoendana na mazingira ya sasa kibiashara.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Vikokotoni Zanzibar Juma Said, alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kushirikiana vizuri na wafanyabiashara wa eneo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Chama hicho.
No comments:
Post a Comment