MWANASHERIA kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), tawi la Pemba, Bw. Mohammed Masoud akizungumza na wakaazi wa Kijiji cha Mlalashi, Shehia ya Mjanaza, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, hivi karibuni kwenye Mkutano wa wazi uliandaliwa na Idara ya Katiba na Sheria, Zanzibar wakishirikiana na THBUB, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Zanzibar na Shirika la Kimataifa la UNDP. (Picha na THBUB).
Na.Mwashamba Juma - THBUB.
WAKAAZI wa Kisiwa cha Pemba wameshauriwa kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, THBUB ili kupatiwa ufumbuzi.
Wito huo umetolewa na Mwanasheria kutoka THBUB, tawi la Pemba, Bw. Mohammed Masoud wakati akitoa elimu kuhusu majukumu ya Tume hiyo kwenye mkutano wa wazi ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Sheria, Zanzibar uliofanyika katika Kijiji cha Mlalashi, Shehia ya Mjanaza, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, hivi karibuni.
Mwanasheria huyo pia aliwaeleza wananchi wa Pemba kwamba moja ya jukumu la THBUB ni kupokea na kusikiliza malalamiko mbalimbali ya uvunjifu wa haki za binaadamu, bila ya malipo sambamba na kuwaelewesha wananchi hao juu ya umuhimu wa utunzaji wa haki za binaadamu kwa kuzingatia misingi ya utawala bora hasa kuelekea uchaguzi ujao wa 2025.
Aidha, Bw. Masoud aliwasihi wananchi hao kulinda haki zao na haki za watu wengine pamoha na kuwashauri wanakijiji hao kutokua chanzo cha kuvunjiana haki miongoni mwao, ikiwemo kuzifanyia suluhu kesi za udhalilishaji.
“Imekuwa kawaida, kunapotozea kesi za ubakaji kwenye jamii, familia hukaa pamoja na kutafuta suluhu, ikiwemo kuwafungisha ndoa waliodhalilishana, jambo ambalo ni kosa jengine kisheria’’ ameeleza Mwanasheria huyo.
Bw. Masoud pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wakazi wa kisiwa cha Pemba kwenye Ofisi za THBUB ziliopo Chake chake, Mkoa wa Kusini Pemba ili kufikisha malalamiko yao, endapo wakiona kuna haki zao, zimevunjwa.
Akifungua mkutano huo, Sheha wa Shehia ya Mjananza, Hamad Said Ali, amesema ujio wa wanasheria hao katika shehia yake, ni jambo jema ambalo limetoa mchango mkubwa wa uelewa wa masuala ya sheria, kujua majukumu ya THBUB na haki za binadamu.
Kwa upande wake, Mkuu wa divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba, Bakari Ali Omar, aliwasihi wananchi hao kuendelea kuyafikisha malalamiko yao kwa wasaidizi wa sheria, waliomo katika shehia zao hata baada ya kumalizika kwa mikutano hiyo.
Naye, Afisa sheria wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Zanzibar, Salma Bakar Abdulla, alisema mikutano hiyo ya wazi kisiwani Pemba, imelenga kuwafikia wananchi wote na kuwafundisha maana na chimbuko halisi la haki za binaadamu zilikoanzia.
Pia, aliwabainishia wananchi hao kwamba kumebainika kwenye jamii zao kumekuwa na uvunjivu wa haki za binaadamu, kwa kujua ama kutokuelewa ndio maana, Idara hiyo kwa kushirikiana na mshirika wake Shirika la kimataifa la UNDP, wamekuwa na utaratibu wa kuwafikia wananchi moja kwa moja.
“Ni vyema wananchi mzitumie fursa za mikutano kama hii, kwa kuuliza na kupata ufafanuzi juu ya changamoto za kisheria mnazokabiliana nazo, zikiwemo vyeti vya kuzaliwa, migogoro ya ardhi na masuala ya kulipwa fidia,’’alifafanua Mwanasheria huyo.
Mikutano mengine kama hiyo ilifanyika kwa baadhi ya shehia kisiwani Pemba, zikiwemo Shehia za Mbuzini na Mchanga Mrima za Wilaya ya Chakechake, na Shehia za Mgagadu na Minazini kwa Mkoa wa Kusini Pemba.
Aidha, Sheia nyengine zilizoitishwa mikutano hiyo kwa upande wa Kaskazini, Pemba ni Shehia za Msuka Magharibi na Mashariki, shehia ya Kiuyu Wilaya ya Micheweni na Shehia za Shengejuu na Mjanaza kwa Wilaya ya Wete. Iliratibiwa na Idara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na THBUB, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Zanzibar na Shirika la kimataifa la UNDP,
MWISHO.
No comments:
Post a Comment