Habari za Punde

utambulisho wa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (CHW) ni hatua muhimu kwa Serikali



 

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa amesema utambulisho wa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (CHW) ni hatua muhimu kwa Serikali itasaidia kurahisisha huduma za Afya na kupunguza maradhi na vifo vya mama na mtoto kwa wananchi wa Zanzibar.

Ameyaeleza hayo katika hafla ya utambulisho na makabidhiano ya Wahudumu wa Afya ya jamii (CHW) kutoka Wizara ya Afya Zanzibar kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi iliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni Zanzibar ambapo amesema wahudumu hao ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali na uimarishaji wa afya ya mama na mtoto.

Amesema dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuwapandisha hadhi wahudumu hao kutoka kujitolea (CHV) hadi kuwa wafanyakazi ni sehemu ya juhudi kubwa katika kuona wananchi wanapata huduma bora za Afya kwa wakati kuanzia ngazi ya afya ya jamii hadi ngazi za rufaa.

Amewahimiza wahudumu hao kufanya kazi kwa weledi na ufanisi kwa lengo la kufikia malengo ya Serikali ya kuiwezesha jamii kuzifikia huduma za Afya kwa haraka kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na mikoa katika kulifanikisha jambo hilo.

Mbali na hayo amewataka wahudumu hao kuwa waadilifu kwa kufanya kwa mujibu wa taratibu ili kujenga jamii iliyobora na kuahidi kushirikiana nao bega kwa bega ili kufanikisha azma ya Serikali katika sekta ya afya.

Aidha, amewapongeza viongozi wa Wizara ya Afya kwa mchango wao katika kuwaendeleza wahudumu hao na kusimamia mchakato wa kuwatambulisha pamoja na kuwakabidhi kwa viongozi wa Mkoa na Serikali za mitaa hatua itakayokuza maendeleo ya huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amesema nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa katika huduma za afya kupitia mfumo wa kinga kwa kutumia wahudumu wa Afya wa Ngazi ya jamii hivyo ni wakati wa wahudumu hao kubeba jukumu hilo kama nguzo ya kwanza ya uimarishaji wa huduma bora za afya katika jamii.

Ameongeza kuwa jukumu jingine la CHW ni kuimarisha uelewa wa afya kwa jamii kwa kila kaya, shehia na wilaya, sambamba na kutoa elimu ya kinga pamoja na uchunguzi wa awali na rufaa pale inapohitajika.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohammed amesema mpango wa kuwatambua CHW ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. Mwinyi ambapo kwa sasa jumla ya wahudumu wa afya ya jamii ni 651 katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao wamehitimu mafunzo ya miezi sita ambao wameanza kufanya kazi za kijamii.

Amefafanua kuwa kwa sasa CHW watakuwa chini ya usimamizi wa viongozi wa Mikoa na Wilaya wakijikita katika kutoa elimu ya afya pamoja na kushiriki katika kampeni za kijamii, kupinga unyanyasaji wa kijinsia, kushiriki katika tafiti za afya jambo litakalosaidia kupunguza vifo, maradhi mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za afya.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dkt. Salim Slim amesema kuwepo kwa CHW katika jamii ni sehemu ya kuisaidia Serikali kupunguza kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda kupata matibabu nje ya nchi kwa kuimarisha huduma za kinga huku akiahidi Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana nao ili kupata matokeo chanya.

Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii Halima Ali khamis ameeleza kuwa hadi sasa jumla ya wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Elfu moja mia mbili na Arubaini na mbili (1,242) wamemaliza mafunzo yao huku zaidi ya Elfu moja na Hamsini na nne (1,054) wakiendelea na mafunzo ikiwa ni sehemu ya uimarihsaji wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo yao.

Mwakilishi kutoka Shirika la la kimataifa la WILLOS Abdul-Wahid Habib pamoja na mwakilishi Mkurugenzi mkaazi wa shirika la kimataifa la D-Tree Anna Mikidadi wamesema CHW ni kiungo muhimu cha kuunganisha kaya na hospitali na kusisitiza kushirikiana na serikali na wadau wengine kutoa huduma bora za afya ya mama na mtoto, huku wakiendeleza matunda chanya kwa jamii.

Kwa sasa Mkoa wa Mjini Magharibi una jumla ya CHW  651 ambapo Wilaya ya Mjini ikiwa na jumla ya CHW 201 tayari wamehitimu mafunzo yao na kuanza kazi, na waliokuwepo kwenye mafunzo jumla ya idadi itafikia 404. Wilaya ya Magharibi “A” ina jumla ya CHW 239 waliomaliza mafunzo na kuanza kazi rasmi na watakapokamilika jumla ya idadi itafikia 549. Aidha, Wilaya ya Magharibi “B” kwa sasa ina CHW 211 waliomaliza mafunzo na kuanza kazi. Na waliokuwepo kwenye  mafunzo jumala ya idadi itafikia 634.

Makabidhiano hayo yaliyombatana na kiapo cha utendaji wa kazi walichopewa CHW na naibu waziri wa afya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.