Habari za Punde

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUMUWAKILISHA RAIS WA ZANZIBAR KATIKA UFUNGUZI WA MSIKITI- FUONI MAMBO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe  kuasiria Ufunguzi wa Masjid Taibah uliopo Fuoni Mambosasa Wilaya ya Magharibi “ B” Unguja, kwa niaba  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-hajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Waumini wa dini ya kiislamu wametakiwa kujitolea kuwekeza katika mambo ya kheri ikiwemo kujenga misikiti, madrasa , sambamba na kuitumia katika  kutatua changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika vijiji vyao.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akimuwakilisha Rais wa zazibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Al-hajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Masjid Taibah uliopo Fuoni Mambosasa Wilaya ya Magharibi “ B” Unguja.

Amesema kuwa kila mmoja kwa nafsi yake anapaswa kufanya mambo mema yatakayosaidia kufikia lengo la kuumbwa kwake hapa duniani  ikiwemo kujenga msikiti, kuchimba visima, kujenga madrasa nayale yote ambayo ni sadakatuljaria kwa umma.

Alhajj Hemed amefahamisha kuwa katika jamii kumekuwa na changamoto mbali mbali hasa kwa upande wa vijana hivyo ni wajibu wa wamumini wa maeneo hayo na maeneo jirani kuutumia msikiti huo kufanyia ibada na kupeana elimu ambayo itawasaidi kufanya ibada kwa uhakika na kuandaa mazingira mazuri ya kesho akhera.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema misikiti ndio sehemu sahihi ya kujadili masuala mbali mbali yanayotokea katika jamii hasa wakati wa swala ya asubuhi na ishaa wakati ambao waumini  hupatikana kwa wingi katika kijiji au shehia ulipo msikiti huo.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza waumini wa dini ya kiislam na wazanzibar kwa ujumla kuendelea kuitunza  amani na utulivu uliopo nchini unaopelekea kufanya harakati mbali mbali za kimaisha hasa wakati huu taifa likielekea katika uchaguzi mkuu wa nchi.

Aidha makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amawataka wazazi na walezi kila mmoja  kutimiza wajibu wake wa kuwalea vijana katika malezi bora yenye kufuata mila silka na tamaduni za kizanzibari.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Mahmuod Mussa Wadi amewataka viongozi wa misikiti kuacha tofauti walizonazo katika suala zima la usimamizi wa misikiti pamoja na kushirikiana katika kufanya ibada jambo ambalo litapelekea kuvurithisha mambo mema vizazi vinavyokuja.

Aidha amewataka waumini  kudumisha usafi na kuutunza  msikiti huo ili kuweza kudumu kwa muda mrefu vizazi hadi vizazi  na kufikia malengo ya ujenzi wa msikiti huo.

Akisoma risala ya ujenzi wa msikiti huo Mkurugenzi wa taasisi ya Al-Noor Charitable Agency for Needy ambayo ndio wafadhili wakuu wa msikiti huo  Sheikh.Nadir Mohammed Mahfoudh amesema kuwa taasisi yao imeshajenga misikiti 42 hadi sasa kwa lengo la kusaidia jamii kufanya ibada na kutoa elimu sehemu sahihi.

Sheikh Nafir amewataka waumini wa msikiti huo kuutumia katia suala zima la kufikisha elimu kwa vijana sambamba  na kuisaidia serikali katika kuhubiri amani na utulivu kwa maslahi mapana ya nchi.

Msikiti huo uliojengwa pamoja na madrasa unatarajiwa kuswaliwa na waumini zaidi ya elfu moja ( 1000) kwa wakati mmoja.


Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..29.08.2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.