WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati zihakikishe kuwa magereza yote nchini yanaunganishwa na mifumo ya nishati safi ifikapo mwaka 2027.
Amesema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuboresha huduma kwa wafungwa, kulinda afya za watumishi na wakazi wa magereza pamoja na kuhifadhi mazingira.
ametoa wito huo leo Jumamosi (Agosti 30, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Magereza nchini. Uzinduzi huo umefanyika kwa niaba ya magereza yote nchini.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa uzinduzi huo ni utekelezaji wa mkakati wa kuhama kutoka nishati zisizosafi na kuhamia katika matumizi ya Nishati Safi ya kupikia. “Rais wetu Dkt. Samia anatambulika Afrika na duniani kwa ujumla kwa hamasa yake ya matumizi ya nishati safi, hatua hii mmeonesha kwa vitendo kwamba mnamuunga mkono”
“Takwimu zinaonyesha kuwa gereza moja linaweza kutumia zaidi ya tani 100 za mkaa kwa mwaka, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60. Kupitia nishati safi, gharama hizi zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50.”
Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kupongeza kwa kuwa inaunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha jamii yote inatumia nishati hiyo na hivyo kwa kiasi kikubwa kuondoa madhara yatokanayo na matumizi ya nishati isiyo safi.
Ameongeza kuwa tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa moshi wa kuni na mkaa una kemikali hatarishi zinazoweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama vile nimonia, kikohozi sugu na pumu. “Kwa kupunguza matumizi ya nishati hizo, Jeshi la Magereza linachangia moja kwa moja katika kuboresha hali ya hewa ndani ya magereza, kuongeza tija ya kazi kwa watumishi na kuhakikisha ustawi wa wafungwa.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Sekta binafsi kuongeza ubunifu na uwekezaji katika teknolojia nafuu na salama za kupikia, ili kuharakisha upatikanaji wa suluhisho bora kwa wananchi wengi zaidi.
“Pia Wizara ya Fedha na Viwanda na Biashara hakikisheni mnaweka mizania rafiki ya kisera, kodi na mifumo kwenye uwekezaji wa Nishati Safi ya kupikia. Kadhalika Kila Taasisi, Kila Jamii, na Kila Mwananchi ana jukumu katika matumizi ya nishati safi. Tuchukue hatua leo, kwa manufaa ya kesho ya watoto wetu na vizazi vijavyo”.
Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo amesema kuwa mradi huo uliozinduliwa utasaidia sana katika utunzaji wa mazingira na wapishi katika magereza nchini. “Jeshi letu la magereza limefanikiwa kutekeleza kwa asilimia 100 matumizi ya nishati safi kwenye magereza”.
Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu amesema kuwa kwa miongo mingi Jeshi la Magereza limekuwa likitumia kuni kama nishati ya kupikia na mahitaji ya kuni yalikuwa ni wastani wa mita za ujazo 91,391.25 kwa mwaka.
Amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2024 Magereza yote nchini yalikuwa yameshaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya chakula cha wafungwa na mahabusu. “Mpaka sasa vyanzo vya nishati mbadala vinayotumika katika magereza ni Gesi Vunde (BIOGAS), Mkaa Mbadala (Briquettes), Kuni Poa na Gesi Asilia (NATURAL GAS).”
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Nishati Vijijini (REB) Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema kuwa Wakala wa Nishati vijijini walisaini mkataba wenye thamani ya shilingi bilioni 35.2 kwa ajili ya utoaji ruzuku ya kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa magereza yote Tanzania.
“Sisi REA tunatoa shilingi bilioni 26.5 sawa na asilimia 75.4 na Jeshi la Magereza linachangia shilingi bilioni 8.6 sawa na asilimia 24.6”
Amesema fedha hizo zitatumika kujenga miundombinu 126 ya biogas na majiko banifi 377, ujenzi wa miundombinu 64 ya LPG na majiko banifu 256, usambazaji wa mitungi ya gesi 15, 126 ya kilo 15, ununuzi wa mashine 61 za kutengenezea mkaa mbadala kwa kambi 22 za Jeshi la Magereza pamoja na kusambaza makaa ya mawe tani 865 na majiko banifu 344.
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Msimamizi wa Kitengo cha Kilimo, Mifugo na Utunzaji wa Mazingira kutoka Jeshi la Magereza SACP Daimu Mmolosha amesema lengo la jeshi hilo ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha nishati ili kuepukana na matumizi ya kuni ma mkaa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 30, 2025
No comments:
Post a Comment