Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Masoud Juma Haji amesema Taasisi ya Pamoja Youth Initiative (PYI) inaendelea kuwapatia mafunzo vijana wa Kizanzibar ili kutambua vipaji vyao na kuvielekeza katika maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumza katika hafla ya utambulisho wa Mradi wa “Sauti Yetu” uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Migombani – Masoud amesema ushirikiano kati ya Wizara na PYI utasaidia kuwafikia vijana wengi zaidi katika mikoa mitatu ya Unguja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PYI Rashid Mwinyi amesema mradi huo unalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika vyombo vya maamuzi na masuala ya siasa, sambamba na kutoa elimu ya uraia, utawala bora na haki za kidemokrasia.
Ameeleza kuwa kutakuwa na makongamano, mijadala, pamoja na mafunzo maalum kwa vijana walioko katika nafasi za uongozi ndani ya vyama vya siasa na asasi za kiraia.
Aidha, amesema mradi huo pia utawajengea uwezo waandishi wa habari kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi.
Mradi wa Sauti Yetu unatekelezwa kwa muda wa miezi tisa hadi mwezi Aprili mwaka 2026 na umefadhiliwa na shirika la Forum Syd kutoka Sweden.
No comments:
Post a Comment