Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Kitaifa, yanayotarajiwa kufanyika Julai, 7 mwaka huu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk.Husein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya  Kiswahili Kitaifa, yanayotarajiwa kufanyika Julai, 7 mwaka huu katika Ukumbi wa Polisi Ziwani.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab wakati akizungumza na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali kuhusiana na Siku ya Kiswahili kitaifa huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.

Amesema kwa mwaka wa 2025, Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani, yataadhimishwa Zanzibar kwa shughuli, zinazohusiana na lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mswahili katika maeneo mbali mbali.

Aidha ameeleza kuwa, Mkutano huo, utajadili kwa kina masuala yanayohusu Kiswahili ambapo Washiriki wataongeza maarifa na ujuzi wa umuhimu wa usomaji wa vitabu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akitaja ratiba ya baadhi ya shughuli zitakazotarajiwa kufanyika amesema kuwa, mnamo Julai 05 ,2025 katika Hoteli ya New Amaan Complex kutafanyika Jukwaa la Mwanamke hazina na kuwasiliswa Makala ya Mwanamke na Utawala bora, Taswira ya Mwanamke Kiongozi katika Fasihi, Vijana wa Kike na Uongozi wa Kesho pamoja na Uwekezaji kwa Kizazi kijacho.

Aidha amefahamisha kwamba, Julai 06, kutakuwa na matembezi ya Wanafunzi na Wadau wa Kiswahili, yatayoanzia Skuli ya Sekondari Tumekuja na kumalizikia Ukumbi wa Ziwani Polisi ambapo pia kutawasilishwa Makala ya Umuhimu wa usomaji wa vitabu sambamba na kutolewa Tunzo kwa Washindi wa mashindano ya Insha kwa Skuli za Sekondari, 2025 sambamba na kukabidhiwa Tunzo Wanafunzi bora wa mwaka 2024 na Mgeni Rasmi anatarajiwa  kuwa Waziri wa Habari , Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar Dk. Mwahija Ali Juma amesema Wazanzibar wengi ni wagumu kusoma vitabu jambo ambalo linachangia kupotea kiswahili cha Unguja Mjini kwa kushindwa kukiendeleza na kukiuza kiswahili sambamba na kupoteza Mila, Silka na Tamaduni za Mzanzibar.

Mnamo June 28,2025 kumefanyika mbio za masafa za Kimataifa za Kiswahili katika Mkoa wa Arusha, zenye kauli mbiu kiswahili fahari ya afrika, zikiwa ni mbio za kilo mita 5,10,15,20.

Tarehe 23, Novemba mwaka 2021, UNESCO ilitangaza na kukiweka Kiswahili katika siku maalumu ya Maadhimisho siku ya Kiswahili, kila mwaka ifikapo Tarehe 07, Julai.

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, kwa upande wa Zanzibar, inatarajiwa kufanyika kuanzia Julai, 05 hadi 07, kwa kufanya shughuli mbali mbali zinazohusiana na lugha ya Kiswahili.

Imetolewa na Kitengo cha Habari,

WHVUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.