Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefungua Kongamano la Amani Mkoani Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali itaendelea kuhakikisha amani na mshikamano uliopo nchini unadumu na kuimarika zaidi.

Ameyasema hayo wakati wa  ufunguzi wa kongamano la kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 lililofanyika katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani kisiwani Pemba.

Amesema amani na mshikamano ndio nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo na bila ya amani hakuna maendeleo yatakayofikiwa na badala yake ni uharibufu wa miundombinu na watu kupoteza maisha yao na mali zao.

Mhe. Hemed amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ikiwemo uimarishaji wa sekta elimu, afya, barabara, maji safi na salama, bandari, masoko na uimarishaji wa maslahi ya wafanyakazi, yamesaindia kwa kiasi kikubwa  kuongeza ustawi wa wananchi.

Aidha, amefahamisha kuwa mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na viongozi bora na kuwepo kwa amani na mshikamano ambao ni nyenzo muhimu ya kuyafikia malengo na maono ya viongozi wakuu wa nchi.

Ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wakati wote wanatumia kauli zitakazodumisha umoja na mshikamano na sio kuchochea, kuwagawa watu na kuvuruga amani.

Sambamba na hayo, amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani kwa waumini wao pamoja na kuwaomba wazazi kuwaelimisha vijana kutokubali kutumika kuwa chanzo cha uchafuzi  wa amani kwa maslahi ya watu wachache wasioitakia mema Zanzibar kwa kutumia kisingizio cha uchaguzi mkuu.

Amewakumbusha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa weledi na kufuata misingi na maadili ya kazi zao kwa kutoa taarifa zitakazohamasisha amani na mshikamano.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Rashid Hadid Rashid amesema Amani ni miongoni mwa tunu kubwa na urithi wa Taifa letu hivyo ipo kila sababu ya kuilinda na kuidumisha amani iliyopo nchini ambayo ikitoweka ni vigumh kuweza kuirudisha.

Hadidi amesema siasa za chuki zimepitwa na wakati na hazijawahi kujenga wala kuleta maendeleo katika nchi yoyote duniani hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vipo makini katika kuhakikisha amani inaendelea kudumu na wananchi wanaendelea na harakati za ujenzi wa Taifa  wakati wote.

Amemuhakikishia Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Mkoa wa Kusini Pemba upo salama na wanajipanga katika kuhakikisha amani inatawala katika kipindi chote cha harakati za uchaguzi  Mkuu na baada ya uchaguzi na hawatokuwa tayari kuona mtu ama kikundi cha watu kikichafua amani iliyopo nchini.

Nae Mratibu wa Kongamano hilo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki amesema lengo la kongamani hilo ni kuzileta pamoja taasisi mbali mbali kuweza kuhamasisha mshikamano na  kujadili namna bora ya kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini.

Amesema mijadala itakayojadiliwa katika kongamano hilo itatoa matokeo chanya juu ya kudumisha amani na utulivu uliopo nchini ili kutoa nafasi kwa viongozi na wananchi kuendeleza harakati za kimaendeleo kabla na baada ya kumalizika kwa uchaguzi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Miza amefahamisha kuwa ujenzi wa amani ni kazi ya pamoja bila ya kujali dini, jinsia ama nafasi ya mtu katika jamii bali kila mmoja wetu kwa nafasi yake anatakiwa kuhamasisha amani na kuidumisha ili iweze kurithiwa na vizazi vilivyopo na vijavyo. 

Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abulla akizungumza na wananchi pamoja na viongozi kutoka sehemu mbali mbali katika ufunguzi wa kongamano la kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 lililofanyika katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani kisiwani Pemba.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR )

Tarehe 06.09.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.