STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29.09.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongezwa kwa
juhudi zake za kuwawekea mazingira bora wafanyakazi wa sekta ya umma yakiwemo
maslahi yao, mafunzo pamoja na vitendea kazi.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid Salum aliyasema hayo leo katika
ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi katika hotuba yake ya ufungaji wa
mafunzo ya mapishi na ukaribu yalioendeshwa na wakufunzi kutoka Taasisi ya
“China National Research Institute of Food and Fermentation Industries”, ya
nchini China.
Katika maelezoa yake Katibu Mkuu huyo alisema kuwa
Mafunzo hayo ni kielelezo cha dhamira njema ya Rais Dk. Shein ya kuwajengea
uwezo watumishi ili kutoa huduma zilizo bora zaidi na kuacha tabia ya kufanya
kazi kwa mazoea “Business as Usual”.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yamejenga daraja
jengine la ushirikiano na uhusiano mwema kati ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na wananchi wa nchi
mbili hizo.
Aliongeza kuwa Jamhuri ya Watu wa China imeendelea
kuwa na mahusiano ya kidugu na ya kihistoria na watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa jumla ambapo nchi hiyo imeonesha jitihada kubwa katika
kutoa fursa za kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali na viongozi kwa kuwapa
mafunzo mbali mbali nchi mwao.
Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kutoa
shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kukubali ombi la Rais
Dk. Shein la kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo watumishi
wanaotoa huduma za mapishi na ukarimu katikaOfisi za Viongozi Wakuu wa nchi
pamoja na Walimu wa Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kutoa
wito kwa wafanyakazi waliopata mafunzo hayo, kuthamini fursa hiyo adhimu na
adimu waliyoipata kwa niaba ya watumishi wengine na kufanyakazi kwa bidii na
nidhamu ili waoneshe mabadiliko ya ufanisi katika shughuli zao za kazi.
Pia, alitoa shukurani maalum kwa uongozi wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa
ushirikiano wao na kukubali kuendesha mafunzo hayo katika taasisi ya Chuo cha
Utalii Maruhubi, Zanzibar.
Sambamba na hayo, Katibu Mkuu huyo, alitoa
shukurani kwa Wakufunzi wa mafunzo hayo na Taasisi ya “China National Research
Institute of Food and Fermentation Industries” kwa kufanikisha utoaji wa
mafunzo ya mapishi na ukarimu kwa watumishi wa Ofisi za viongozi wakuu wa
Zanzibar pamoja na walimu wa Chuo cha Utalii, Maruhubi Zanzibar.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa
na Biashara wa Taasisi ya “Chaina National Institute of Food and Fermentation
Industries” Bibi Luo Yanqin alieleza kuwa mafunzo hayo yameenda vizuri na
kuwapongeza watendaji wote walioshiriki mafunzo hayo.
Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuisifu
Zanzibar pamoja na mazingira yake yakiwemo mazingira ya kitalii, fukwe, misitu,
mazao ya viungo, ukarimu wa watu wake, maeneo ya kihistoria pamoja na mambo
mengineyo ya kuvutia.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa
mafunzo hayo yamezidi kuw chachu ya mahusiano na mashirikiano mema kati ya
Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar.
Nao watendaji hao waliopata mafunzo hayo walitoa
shukurani maalum kwa Rais Dk. Shein kwa kuwaandalia mafunzo hayo muhimu ili
kuwajengea uwezo katika kuzitekeleza vyema kazi zao.
“Tunamwambia ahsante na Mwenyezi Mungu amjaalie
kila la kheri, aidha, tunatoa shukurani kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa kuyaratibu
mafunzo yetu”, walieleza watendaji hao katika hotuba yao iliyosomwa na Mustafa
Ahmada Ali ambaye ni miongoni mwa watendaji waliopata mafunzo.
Sambamba na hayo, watendaji hao walitoa ombi maalum
la kuongezwa muda wa mafunzo hayo mara nyengine kwani mafunzo hayo yaliokuwa na nadharia na
vitendo yamewapa maarifa mapya na ujuzi wa kuongeza ufanisi wa kazi zao huku
wakiwapongeza wakufunzi walioendesha mafunzo hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment