STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dubai 26.01.2018

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein
amekutana na Umoja wa Wanawake wa Dubai (DWE), na kufanya nao mazungumzo ambapo
Umoja huo umeahidi kuwaunga mkono akina Mama wa Zanzibar wakiwemo waliojiunga
kwenye vikundi ili wazidi kupata maendeleo endelevu sambamba na kujikwamua
kiuchumi.
Mama Shein alikutana na
Umoja huo wa Wanawake wa Dubai (DWE), mjini Dubai ambao katika maelezo yake
Mama Shein aliueleza Umoja huo mafanikio yaliofikiwa na wanawake wa Zanzibar
pamoja na changamoto walizonazo.
Katika maelezo yake Mama
Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa katika
kujiletea maendeleo yao.
Mama Shein alieleza kuwa
chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein wanawake wameweza kupewa fursa nzuri katika uongozi Serikalini
pamoja na kupewa vipaumbele kwenye masuala mbali mbali ya kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Alieleza kuwa Umoja wa
Wanawake wa Tanzania (UWT), kwa upande wake umekuwa ukitoa mashirikiano na
kuwasaidia wanawake wenzao sambamba na kuwaunga mkono akina mama walioko mjini
na vijijini kwa kuwasaidia katika miradi yao ya maendeleo kupitia vikundi vyao
walivyoviunda.
Mama Shein alieleza kuwa
kwa upande wa Zanzibar wanawake wengi ambao wameunda vikundi vyao wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mafunzo na utaalamu ambao
utawasadia katika kuendeleza miradi yao.
Aidha, Mama Shein
alieleza kuwa wanawake wa Zanzibar wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa soko la
kuuzia bidhaa zao wanazozitengeneza pamoja na ukosefu wa vifaa vya kutendea
kazi zao katika vikundi vyao walivyoviunda.
Kutokana na Umoja huo
kuonesha nia ya kuwasaidia wanawake wa Zanzibar, Mama Shein alieleza haja ya
uongozi wa Jumuiya hiyo kuitembelea Zanzibar na kupata fursa ya kuvitembelea
vikundi vya wanawake wa Zanzibar ili kujionea wenyewe mafanikio yaliofikiwa
sambamba na changamoto wanazozikabili.
Sambamba na hayo, Mama
Shein ameeleza haja ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya Umoja huo na Umoja
wa Wanawake wa Tanzania (UWT), ikiwa ni pamoja na viongozi wake kutembeleana
kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya pande mbili hizo.
Nao Umoja wa Wanawake wa
Dubai (DWE) ulimuahidi Mama Shein kuwa uko tayari kuwaunga mkono akina mama wa
Zanzibar sambamba na kushirikiana nao kikamilifu huku ukisisitiza kuwa mara
baada ya taratibu za kidiplomasia zitakapokamilika wako tayari kuitembelea Zanzibar
kwa lengo la kukutana na akina mama wenzao.
Akina Mama hao
walimueleza Mama Shein kuwa Umoja wao una fursa mbali mbali ambazo zinaweza
kuwasaidia akina mama wa Zanzibar hasa wale ambao wamejiunga katika vikundi
kutokanan na uzoefu na utaratibu walionao wa kuwasaidia katika Nyanja zote.
Walieleza kuwa Umoja wao
pia umekuwa ukitoa fursa mbali mbali
ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo, misaaada ya kifedha na kitaalamu pamoja
na vifaa jambo ambalo wako tayari kulifanya kwa akina Mama wa Zanzibar kwani
wamevutika na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jinsi
inavyowaunga mkono wanawake.
Aidha, akina mama hao wa
Umoja wa Wanawake wa Dubei (DWE), ambao uko chini ya kiongozi wake Mke wa
Mtawala wa Dubai Mama Sheikha Manal Bint Mohammed Bin Rashid Al Maktoum,
uliahidi kukuza ushirikiano wake na uhusiano wa karibu uliopo kati ya pande
mbili hizo.
Sambamba na hayo,
uongozi wa Umoja huo nchini Dubai ulitumiafursa hiyo kumpongeza Mama Shein kwa
kuwatembelea pamoja na kupata kujua shughuli zao na kueleza kuwa hatua hiyo ya
Mama Shein inaonesha wazi jinsi anavyowajali, anavyowasamini na kuwapenda akina
mama wenziwe ambao na wao kwa uoande wao wamemuhakikishia kuwa wataendelea
kumpenda na kumthamini na kumuweka katika kumbukumbu zao.
Umoja huo umeundwa mwaka
2006 chini ya Sheria Namba 26 na kutangwazwa rasmi mnamo mwaka 2008, kupitia
Mtawala wa Dubai Sheikh Mohammed Bin
Rashid Al Maktom.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment