Habari za Punde

NAIBU WAZIRI MHE.KANYASU AWATAKA WANANCHI WANAOISHI NDANI YA HIFADHI YA MISITU KULIPA TOZO BILA SHURUTI
















Na.Lusungu Helela - Mwanza.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu amewataka wananchi wanaoishi na kufanya shughuli za uzalishaji mali ndani  ya Hifadhi ya misitu ya Visiwa vya  Kome  na Maisome vilivyoko wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza kulipa tozo za serikali bila kulazimishwa.

Kauli hiyo ameitoa  wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya  Msitu wa Shigala ulioko Kome Mchangani ambayo ni kambi ya wavuvi wakati alipofanya ziara ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Mbunge wa Jimbo la Buchosa Dkt. Charles Tizeba amemueleza  Naibu Waziri hiyo kuwa kumekuwepo na changamoto ya ulipaji  tozo kubwa hata kama mtu ana eneo dogo na ndipo wananchi walilazimika kugoma kulipa tozo hiyo kwa lengo la kupata msaada zaidi.

Amefafanua kuwa mtu anayemiliki hekari moja  anatakiwa kulipa Tsh.425,000 kwa mwaka lakini hata mtu anayemikili eneo dogo la mita 20 naye anatakiwa kulipa kama wa hekari moja  kitendo kilichowafanya wananchi hao kushindwa kulipa na kusubili maelekezo ya wizara husika.

Mmoja wa wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi hiyo,Juma Ramadhani amemwomba Naibu Waziri kuangalia upya sheria hiyo ili wananchi wapate nafuu ya kulipa na serikali iweze kupata mapato yake.

Kaimu Meneja wa TFS Kanda ya Ziwa, Thomas Moshi amesema kuwa tozo hizo zipo kwa mujibu wa sheria kinachotakiwa ni wananchi kulipa na siyo kugomea kulipa tozo hizo na wanapofanya hivyo wanakwenda kinyume na matakwa ya sheria ya hifadhi ya misitu.

Kanyasu amewahakikishia wananchi hao kuwa suala hilo atalipatia majibu kwa haraka lakini amewataka watu wanaomiliki hekari moja  kulipa tozo hizo kwa wakati na wale wenye maeneo madogo madogo wajiunge katika vikundi ili waweze kuilipa pesa hiyo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.