Habari za Punde

Uratibu wa Shughuli za Serikali Umelenga Kuwaondoshea Usumbufu Wananchi Wanaoishi Upande wa Tanzania Bara.

Mratibu Mkuu wa Uratibu wa Shughuli za SMZ  Dar es salaam Nd. Issa Mlingoti Ali Kushoto akisalimiana na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa huku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifurahia wakati walipofika Nyumbani kwake Dar es salaam kutambulishwa Rasmi baada ya kuteuliwa kuwa Mratibu Mkuu.
Mratibu Mkuu wa Uratibu wa Shughuli za SMZ  Dar es salaam Nd. Issa Mlingoti Ali akisalimiana na baadhi ya Mabalozi wa Nchi za Nje waliopo Tanzania wakati akiwa katika ziara za kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi hizo za Kidiplomasia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mratibu Mkuu wa Uratibu wa Shughuli za SMZ  Dar es salaam Nd. Issa Mlingoti Ali akisalimiana na baadhi ya Mabalozi wa Nchi za Nje waliopo Tanzania wakati akiwa katika ziara za kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi hizo za Kidiplomasia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Wakati umefika kwa Watanzania wote kuitumia Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Dar es salaam ili kupata maelekezo na Ushauri utakaowawezesha kupata huduma mbali mbali zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ngazi na Sekta zote.
Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuanzisha Ofisi hiyo muhimu Mwaka 2013 kuratibu wa Shughuli za Serikali umelenga kuwaondoshea usumbufu Wananchi wanaoishi upande wa Tanzania Bara pamoja na Taasisi za Kimataifa zinazohitaji huduma za Serikali.
Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Dar es salaam Ndugu Issa Mlingoti Ali alitoa kauli hiyo katika Kipindi Maalum cha matayarisho ya maandalizi ya sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 hapo Ofisini kwake Mjini Dar es salaam.
Ndugu Mlingoti alisema huduma za Ofisi hiyo kwa kiasi kikubwa hivi sasa zinatumiwa zaidi na Viongozi Wakuu na wale Waandamizi jambo ambalo bado halijakidhi azma ya kuanzishwa kwake licha ya kwamba yapo mambo mengi na ya msingi yanayoweza kuratibiwa ambayo yanamuhusu pia Mwananchi wa kawaida.
Alisema Ofisi hiyo kupitia Maafisa wake wa Sekta Tofauti ina mamlaka ya kusikiliza na kuyachukulia hatua matatizo yanayowakumba Wananchi sambamba na kuwa kiunganishi cha mawasiliano ya ushirikiano baina ya Taasisi za SMS na zile za Tanzania Bara pamoja na za Kimataifa katika Sekta tofauti.
Mratibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es salaam alifahamisha kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kwa Ofisi hiyo ndani ya Awamu ya Saba ya Uongozi wa SMZ ambayo yanafaa kuendelezwa.
Nd. Mlingoti alitolea mfano uchelewaji wa malipo ya masomo kwa baadhi ya Wanafunzi wa Zanzibar wanasoma Vyuo tofauti vya Tanzania Bara pamoja na changamoto iliyowapata Wafanyabiashara wa Maboti ambapo Ofisi ilifanikiwa kukabiliana na changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi licha ya ukosefu wa Bajeti Maalum.
Alisema katika kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa Kimataifa Uongozi wa Ofisi hiyo tayari umeshazitembelea Ofisi za Kibalozi 18 na Jumuiya Tatu za Kimataifa ziara ambayo pamoja na mambo mengine yalifanyika mazungumzo na kuleta mafanikio kwa SMZ.
“ Tumeshatembelea na kufanya mazungumzo ya ushirikiano na Uongozi wa Ofisi za Kibalozi za Ireland, Bahrain, Switzerland, Afrika Kusini, Namibia, Italily, Sweden, Norway, Brazil, Japan, na Taasisi za Kimataifa za  Jica, Juice na Looks”. Alisema Mratibu Mkuu huyo wa Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es salaam.
Ndugu Mlingoti alifahamisha kwamba hatua hiyo imepelekea Ofisi ya Uratibu kuingizwa katika Kamati Maalum ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japan chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Japani {JICA}.
Alisema Kamati hiyo tayari imeshaanzisha Mpango wa kuwaendeleza Watanzania kupata fursa za ajira pamoja na nafasi za masomo katika ngazi ya Shahada kwenye vyuo mbali mbali Nchini Japani ambapo Zanzibar tayari imeshafanikiwa kupata Wahitimu Wanane katika Awamu Nne tokea kuanzishwa Mpango huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.