Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed ajumuika na Waislamu kwenye sala ya Ijumaa Msikiti wa Ijumaa Mwacha Alale Mfenesini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilisha Ibara ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kijiji cha Mwache Alale Jimbo la Mfenesini Wilaya ya Magharibi A.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kijiji cha Mwache Alale Jimbo la Mfenesini Wilaya ya Magharibi A.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed hayupo pichani wakati akisalimiana nao baada ya sala ya Ijumaa.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mh. Machano Othman Said  akibadilishana mawazo na Mhe. Hemed nje ya Msikiti wa Ijumaa wa Mwache Alale baada ya kumaliza sala ya Ijumaa Kijijini hapo.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewapongeza Waumini wa Imani za Dini pamoja na Wananchi Nchini kwa utulivu wao mkubwa unaotoa faraja kwa Serikali Kuu kuendelea kujipanga katika kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wakati akitoa salamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kijiji cha Mwache Alale Jimbo la Mfenesini Wilaya ya Magharibi A Mh. Hemed alisema nguvu za pamoja zinahitajika ambazo ndio msingi pekee wa kuelekea kwenye mafanikio ya maendeleo yatakayonufaisha Serikali na Wananchi wake.

Alisema maendeleo hayo yatafikiwa na kupatikana endapo nyoyo za Wananchi zitalelewa katika kuepuka Fitina, chuki, Uhasama na Ubaguzi mambo ambayo hata katika Vitabu na Miongozo ya Dini zote yamekuwa yakipigwa vita na kutopewa nafasi ya kutawala ndani ya nafsi za Watu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Waumini na Wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali yao kwa kushiriki kwenye vita dhidi ya vitendo vya Rushwa na udhalilishaji wa Kijinsia vinavyoonekana kuitia doa Zanzibar.

Alitahadharisha kwamba hayo si mambo ya kuyachezea kwa vile yanaendelea kuvitia dosari Visiwa vya Unguja na Pemba vilivyoshiba Utamaduni wa Ukarimu wa Watu wake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwamba maamuzi yanayochukuliwa na Serikali Kuu katika kipindi hichi cha mpito baadhi ya Wananchi yatawagusa lakini cha msingi ni kuwa na moyo wa uvumilivu utakaotoa majibu sahihi bila ya kumuonea Mwananchi.

Akitoa Shukrani Mwakilishi wa Waumini na Wananchi wa Kijiji cha Mwache Alale Mzee Ameir amemthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wao  wako pamoja na maamuzi yanayochukuliwa na Viongozi wao mambo ambayo waliyatarajia kutokana na kasi ya uwajibikaji wa Serikali.

Mzee Ameir  alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi asiwe na wasi wasi na Wananchi wa Kijiji cha Mwache Alale na kumtaka aendelee kuziba viraka  vilivyoachwa na baadhi ya wakorofi waliojilimbikizia Mali za Umma kinyume na utaratibu.

Mwakilishi wa Waumini na Wananchi hao wa Kijiji cha Mwache Alale alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia changamoto zinazowakabili Wananchi hao za ubovu wa Bara bara iendayo Kijiji hicho inayoviza maendeleo yao hasa huduma za Kielimu kutokana na Walimu kuchelewa madarasani.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.