Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi aagiza kuchukuliwa hatua kwa viongozi walioshindwa kurejesha fomu la Tamko la Rasilimali na madeni kwa wakati

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar
                         

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma kujiridhisha ili kubaini sababu za msingi za Viongozi 52 kushindwa kurejesha Fomu za Tamko la Rasilimali na madeni kwa wakati uliowekwa  na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria.

 Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakili, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

 Alisema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 jumla ya Viongozi 2578 walichukua Fomu za tamko la Rasilimali na madeni ambapo Viongozi 2556 walirejesha fomu hizo  kwa wakati muafaka, huku Viongozi 52 wakirejesha  fomu hizo nje ya muda uliowekwa.

 Alisema viongozi waliorejesha fomu hizo nje ya wakati uliowekwa ni namna ya viongozi  wanaopewa kazi na kuacha kuzifanya na pale inapotokea wakafanya  hukamilisha kwa wakati wanaopenda wao wenyewe.

 Dk. Mwinyi aliwakumbusha Viongozi wote wa Umma waliotajwa katika sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuhakikisha wanarejesha Fomu hizo baada ya kuzijaza sio zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2021.

 Akigusia tatizo la baadhi ya Viongozi katika kujaza fomu hizo eneo linalohusu Mapato ya biashara, Dk. Mwinyi alisema fomu mpya iliofanyiwa marekebisho ambayo itatumika mwaka huu imezingatia suala hilo, hivyo akawataka viongozi kuijaza  vizuri ikiwa na taarifa zote muhimu zinazohitajika.

 Alitumia fursa hiyo kuipongeza Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuwa na  mashirikiano na Vyombo mbali mbali vya Habari na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi na majukumu ya Tume hiyo na namna bora ya kuwasilisha malalamiko yao na akabainisha kuwepo wananchi wengi wnaotumia taasisi hiyo kwa lengo la kuimarisha Utawala bora.

 Aliutaka uongozi wa taasii hiyo kuendeleea kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, udhalilishaji, mgongano wa kimaslahi na tuhuma za rushwa na wizi pamoja na vitendo visivyoridhisha katika jamii,nae akaahidi kuzizfanyia kazi kwa haraka.

 Aidha, Dk. Mwinyi aliwataka Viongozi wote waliowateuwa kuwa na utaratibu wa kumpa taarifa za mara kwa mara juu ya hatua walizozichukua dhidi ya watendaji waliobainika kuhusika na ubadhirifu katika taasisi zao, sambamba akatumia fursa hiyo kuipongeza ZAECA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake vizuri.

 Alisema taarifa zinabainisha katika kipindi cha kaunzia mwezi wa Januari hadi Novemba, 2021 kumekuwepo tuhuma 289 zinazohusiana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ambazo zimechunguzwa.

 ”Hata hivyo nawataka kuongeza kasi ya uchunguzi, kwani taarifa zinaeleza ni majalada 29 pekee ndio yaliowasishwa Ofisi ya DPP”, alisema.

 Alisema katika kuzuia wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, Serikali imeweka mkazo katika kufanya ukaguzi wa fedha za Serikali na akabainisha uwepo wa baadhi ya Viongozi wanaochelewesha au kukwamisha  matumizi ya mifumo mipya ya malipo na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletronik.

 Aidha, alieleza kuwepo kwa  baadhi ya Viongozi wanaokwepa kushirikiana na Ofisi ya  Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali   kwa kushindwa kutoa taarifa muhimu za ukaguzi na kutaka viongozi hao wafichuliwe na kuchukuliwa hatua.

 Raisi Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wananchi kushirikiana katika kujenga maadili na kusema panapo maadili  haki na uwajibikaji hutawala katika ngazi tofauti.

 Rais Dk. Mwinyi alisema ni vyema kwa Viongozi kuitumia siku hiyo kwa kujitathmin na kujipima viwango vya uadilifu na uwajibikaji, uzalendo na utii wa sheria, maadili ya kazi pamoja na madaraka waliyokabidhiwa, sambamba na kutathmin mahusiano yao  na mwelekeo wao katika jamii u

 Alisema amevutiwa sana na kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Piga vita rushwa, heshimu haki za binadamu, uadilifu na Uwajibikaji kwa maendeleo ya Uchumi endelevu’ kwa kigezo kuwa ni ufupisho wa mabo yote ya msingi yanayohitajika katika kuimarisha maendeleo, kudumisha amani, umoja na mshikamano pamoja na ustawi wa kila mwnananchi.

 Alisema utekelezaji wa Utawala Bora bora unahitaji nguzu za pamoja za sekta na wadau wote.

 Nae, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman aliwataka wateule wote wa Rais kufuata mwenendo wa kiutendaji wa Kiongozi huyo pamoja na kumsaidia kikamilifu  ili kufanikisha azma ya kuijenga Zanzibar kwa kuzingatia uzalendo,   uwajibikaji na Uadilifu.

 Waziri Haroun alitumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Jaji Mkuu Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla kwa kuanza kuifanyia mabadiliko chanya Idara ya Mahakama katika kipindi kifupi tangu ashike dhamana hiyo, sambamba na kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji kwa juhudi mbali mbali anazochukua katika utelezaji wa majukumu yake

 Mapema Mwenyekiti, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Asaa Ahmada Rashid alisema Kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Piga Vita rushwa, heshimu haki za binadamu, Uadilifu na Uwajibikaji kwa Maendeleo ya Uchumi Endelevu”inabainisha namna viongozi wa umma na wananchi wanavyopaswa kuwa ili kupata maendeleo ya kweli ya kiuchumi.

 Alisema katika kuimarisha taasisi ziliomo kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbali mbali zinazoongoza taasisi hilo ili ziweze kutekeleza vyema majukumu yake.

 Alieleza kuwa mapambano dhidi ya rushwa, unyanyasaji na uhujumu uchumi, yataweza kufanikiwa pale patapokuwepo mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi hizo na wananchi kwa kuzingatia kuwa wajibu wa kusimamia mapambano hayo hauko kwa taasisi hizo pekee.

                                                                  

Imetayarishwa na Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.