RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwenye nyanja zote za maendeleo, kisiasa, Uchumi, utamaduni na huduma za jamii
yameipatia nchi heshima kubwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi
Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi wakati wa uzinduzi wa Sherehe
za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema,
kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano huo, Tanzania imeendelea kubaki kwenye historia
na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote kutokana na
misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano viliyoasisiwa na viongozi Hayati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano huo.
“Tunaposherekea
miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tuna wajibu wa kujipongeza kwa mafanikio
makubwa nchi yetu iliyoyafikia kwenye nyanja zote za maendeleo kisiasa,
kiuchumi na huduma za jamii. Alisifu Dk. Mwinyi.
Alieleza
dhamira ya dhati kwa viongozi mbalimbali walioshika nyadhifa za uongozi kwa
awamu tofauti kwa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuendeleza maono ya Waasisi wa Taifa hili kumefanikisha kudumisha na kuimarisha
Muungano huo.
“Tunafurahia
kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu kwa
shughuli mbalimbali za maendeleo umeongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea
kudumu” Alisifu Rais Dk. Mwinyi.
Akizungumzia
changamoto za Muungano, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote za
Muungano huo, ikiwemo kuunda Tume na Kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja za
Muungano.
Alisema, miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni
pamoja na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka
2006.
Alisema tangu mwaka huo hadi mwaka huu wa 2024,
hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa, kati ya hoja hizo alieleza hoja 22
zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.
Aidha, hoja zilizobaki Rais Dk. Mwinyi alieleza
kuwa zipo kwenye hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
Dk. Mwinyi pia alieleza Imani yake na kwa utashi wa dhamira ya dhati ya Serikali za pande zote mbili kwamba hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.
“Ni wajibu wetu sote kuulinda, kuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi
ili tuzidi kunufaika sisi tuliopo leo pamoja na vizazi vyetu kwa dhamira ile
ile ya Waasisi wa Taifa letu” Alisihi Rais Dk. Mwinyi.
Alieleza ndani ya kipindi miaka mitatu (2021
-2024) hoja 15 pia zilipatiwa ufumbuzi, kati ya hoja 18 zilizokuwepo.
Alisema, utatuzi wa changamoto za Muungano,
umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zote mbili za SMZ na SMT kwa
kuimarisha na kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu uliopo ambao ni Tunu
muhimu na fahari ya Tanzania
Hata, hivyo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukrani zake
za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha
Muungano na kuwa ni moja ya vipaumbele vyake.
Sambamba na kuwahakikishia Watanzania wote kwamba
Serikali za SMZ na SMT zitaendelea kuchukua hatua ili taifa la Tanzania
liendelee kusonga mbele kwa maendeleo na kuendelea kubaki kuwa nchi ya amani na
utulivu.
Rais Dk. Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuwaomba
viongozi wenziwe na Wananchi wote wa Tanzania kuendelea kuulinda Muungano huo
ili waendelee kuishi kwa amani na kuzidi kujiletea maendeleo binafsi na Taifa
kwa ujumla.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed
Suleiman Abdulla aliwashukuru Rais Dk. Mwinyi na Dk. Samia kwa namna
wanavyoliongoza taifa kwa misingi ya kusimamia Muungano.
Aidha, umuhimu wa kuendelea kulindwa Muungano kuenziwa, kuimarishwa
na kulindwa kwa maslahi ya Watanzania.
Alieleza, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya
Muungano na Mazingira ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanawajibu wa
kuielewaja jamii juu ya historia ya Muungano kwa vizazi viliopo sambamba na
kuwasihi Watanzania kuendelea kuu Watanzania.
Mapema akizungmza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira Dk. Selemani Saidi Jafo alisema historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imeundwa na sababu nyingi hadi kufikia kusainiwa kwa hati ya Muungano mwaka
1964 chini ya waasisi wake Hayati baba wa Taifa Julius K. Nyerere na Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume.
Akitaja baadhi ya sababu hizo zikiwemo urafiki na udugu wa damu wa
Wananchi wa pande mbili za Muungano, lugha ya Kiswahili iliyowaunganisha watu
wa pande mbili hizo, pamoja vyama vya ukombozi vya TANU na ASSP Waziri Jafo
alieleza kwamba vilitoa mchango mkubwa kwenye Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Alisema katika kusheherekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa
Tanzania, Ofisi ya Makamu
wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar wanatarajia kuzindua kitabu maalum kinachoeleza historia ya
Muungano wa Tanzania kwaajili ya kufundishiwa Skuli za Sekondari nchi nzima.
Uzinduzi wa sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Ufunguzi wa Maonesho maalum ya Taasisi za Muungano chini ya kaulimbiu, “Tumeshikamana
na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, unaashiria kuanza rasmi kwa
shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti, usafi wa mazingira na
ushiriki wa wananchi na viongozi kwenye matukio ya uzinduzi wa miradi ya
maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi kwa maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Pia uzinduzi huo
unaashiria hatua za maendeleo kwenye upatikanaji wa fursa kwa Taasisi za
Muungano na zisizo za Muungano, Makampuni na wajasiriamali ili kuionesha jamii
huduma na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika shughuli zao.
Kilele cha sherehe
hizo ni tarehe 26 Aprili, 2024 kwenye viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam ambapo
Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Dk. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
IDARA YA
MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment