WASHIRIKI wa Mkutano wa Mafunzo wa kuwajengea uwezo pamoja na ufanyaji kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia na kuufungua mkutano huo, unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024
WASHIRIKI wa Mkutano wa Mafunzo wa kuwajengea uwezo pamoja na ufanyaji kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia na kuufungua mkutano huo, unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi ametoa wito kwa nchi wanachama za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa bara la Afrika, SADC, kuona haja za kuziimarisha taasisi zao zinazosimamia
utawala bora zikiwemo Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka za
kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi pamoja na Mabunge kuona haja ya kuzipatia
wataalamu zaidi wa fani mbalimbali ili ziwe na upeo mkubwa zaidi wa kufanya
uchunguzi kwa mujibu wa majukumu yao.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alizishauri taasisi hizo kuona
umuhimu wa kufanya ziara za kimafunzo na kujengeana uwezo kwa kujifunza mbinu
bora za kisasa kwenye utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kuendelea kutoa
mafunzo zaidi.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip,
Uwanja wandege Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magaharibi, alipofungua Mkutano wa Mafunzo kwa Wajumbe na Wataalamu wa Kamati za SADCOPAC katika
kupambana na rushwa, kuhamasisha uwazi na uwajibikaji kwa usimamizi wa mali
zisizo rejesheka kwa kamati hizo.
Alisema, Mkutano huo kwa Zanzibar ni fursa nzuri kwa Wataalamu wa ndani pamoja na Mabunge ya nchi wanachama
wa SADC kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na rushwa,
kuongeza uwazi na uwajibikaji kutoka nchi nyengine za mataifa ya Afrika hasa ukanda
wa Kusini mwa Afrika.
Pia alieleza Mafunzo hayo kufanyika Zanzibar ni fursa
ya kuitangaza Tanzania na kuwawezesha wageni kupata nafasi adhimu ya kutembelea
vivutio mbalimbali vya utalii, zikiwemo fukwe nzuri na Mji Mkongwe wa Zanzibar
wenye hadhi ya urithi wa Dunia.
Akizungumzia suala la mapambano dhidi ya vitendo vya
rushwa, kuwepo kwa uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhimiza
uwajibikaji kwenye utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika kukuza uchumi wa mataifa
ya Afrika na kuimarisha huduma za jamii, Rais Dk. Mwinyi alisema ni mambo ya
misingi na yenye mchango muhimu kwa kuchochea kasi ya maendeleo ya mataifa hayo.
Alisema, rasilimali zilizomo Afrika ni vyanzo muhimu
vya kukuza uchumi wa mataifa yao, ikiwa vitasimamiwa vyema na kutumika kwa
misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji. Alisistiza kuwa taasisi za utawala bora zikiwemo Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali, Mamlaka za kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi na Mabunge kwa nchi
wanachama wa SADC yana mchango mkubwa wa kuyafikia matarajio ya mataifa yao.
Alisema, Serikali zote mbili za SMZ na SMZ
zimejitahidi kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na vitendo vya rushwa na
kuhimiza uwazi na uwajibikaji ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
Akitaja hatua hizo Rais Dk. Mwinyi alieleza ni
pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zake kwa mafunzo ili kuzipatia weledi,
kuzipatia vifaa vya kufanyia kazi na kuzijengea miundombinu bora ili zifanye
kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Rais Dk. Mwinyi alisema, inaendelea kupambana na rushwa, kuhimiza uwajibikaji
na uwazi kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ya huduma zikiwemo za kifedha.
Aliongeza, kuanzisha utaratibu wa kusomwa kwa
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hadharani kwa
kujadiliwa kwa kina na uwazi kwenye Baraza la Wawakilishi.
Alieleza, hatua hiyo imeimarisha Mamlaka ya
Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
zimesaidia sana kufikia malengo ya nchi kwa kuimarisha utawala bora.
Akiizungumzia sheria ya Ukaguzi wa Mapato na
Matumizi ya Umma nambari 7 ya mwaka 2023 ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alieleza
imeleta mafanikio makubwa kwenye kujenga uwelewa kwa wananchi juu ya matumizi
ya fedha za Umma.
Kuhusu
mafanikio hayo Rais Dk. Mwinyi alieleza ni pamoja na kutumia mifumo, kuokoa
fedha za Serikali kwa asilimia 86.3, kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi
kwa asilimia 96, kuongezeka kwa uelewa wa usimamizi wa fedha za umma (mapato na
matumizi) kwa asilimia 96, Matumizi ya mifumo kwenye shughuli za Serikali pia
yameongezeka kutoka asilimia 48 na kufikia 92.4
Mafanikio
mengine yaliyopatikana kutokana na kuimarika kwa utendaji huo Rais Dk. Mwinyi
alieleza Serikali ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kupewa
kazi ya kusimamia na kufuatilia matumizi ya miradi ya maendeleo kupitia USAID
na ADB ambapo awali kazi hio ilifanywa na taasisi binafsi.
Hata
hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema, Zanzibar inajitahidi kutekeleza kwa ukamilifu
makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi wanachama wa kamati za SADCOPAC.
“Siku
siku zote tutajitahidi kuwa kinara katika utekelezaji ili malengo na mipango
yetu iweze kufanikiwa kama sote tunavyotarajia” alibainisha Rais Dk.
Mwinyi.Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alizitaka kamati za Mabunge ya nchi
wanachama wa SADC, kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania hasa Zanzibar.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara zinazosimamia sheria na utawala bora Tanzania,
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Zanzibar pamoja na Uongozi na
Sekretarieti ya SADCOPAC.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment