Menu

Monday, May 19, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Akagua Ujenzi wa Kituo cha Maendeleo ya Michezo Malya


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi wa Ujenzi wa chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Peter Naingo,  alipokagua mradi huo akiwa katika ziara ya kikazi mkoa wa Mwanza, Mei 18, 2025.  Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wa tatu kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi , wa nne kulia ni Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na wa tano kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni , Sana na Michezo, Gerson Msigwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza, Mei 18, 2025.  Wa tatu kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi,  wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza Mei 18, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Akademi ya Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya na kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na ujenzi wa mradi huo.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 18, 2025) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo, ambapo amesema Serikali imedhamiria kuendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuwawezesha wananchi kupata maendeleo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ujenzi wa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha wataalamu wengi wa michezo na wanamichezo nchini.

”Serikali itaendelea na ujenzi wa viwanja na vituo mbalimbali vya michezo na miundombinu yake ili kuongeza idadi ya wachezaji wazawa katika timu za mpira wa migu na michezo mingine kama riadha na kuogelea na hivyo tutaweza kuongeza washiriki kwenye michezo mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Olympic.”

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema kiasi cha shilingi bilioni 32.12 kimetengwa na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Akademi ya Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Profesa Kabudi amesema mradi huo unajumuisha ujenzi wa majengo ya madarasa, mgahawa, bweni la wanafunzi, uwanja wa michezo wa ndani na viwanja vya michezo vya nje, ambavyo vyote vitakuwa na viwango vya kimataifa na ujenzi bwawa la kuogelea litakalokuwa na viwango vya Olympic.

Amesema mbali na ujenzi wa viwanja, pia katika chuo hicho zitatolewa diploma za Physical education, ukocha wa michezo na menejimenti ya michezo, lengo likiwa ni kuinua na kukuza vipaji vya michezo nchini. Mradi huo moja ya miradi ya kikakati inayotekelezwa na Serikali kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 37.22.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

JUMAPILI, MEI 18, 2025




No comments:

Post a Comment