Menu

Tuesday, June 17, 2025

SERIKALI YASAINI MIKATABA YA UNUNUZI NA USAFISHAJI DHAHABU

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, akitia saini Mikataba ya Ununuzi na usafishaji madini na Mkurenzi Mtendaji wa  Kampuni ya Madini ya Buckreef  Bw. Isaac Bisansaba, katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma. Halfa ya utiaji saini mikataba hiyo imeshuhudiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde.

Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.


Na. Josephine Majura na Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Benki Kuu ya Tanzania imesaini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu na kampuni za uchimbaji madini na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), hatua itayowezesha Benki Kuu kupata vyanzo vya uhakika katika kufanikisha programu yake ya ununuzi wa dhahabu.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square jijini Dodoma kati ya Gavana wa Benki Kuu na Kampuni za madini wakishuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt.Nchemba alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini ambacho kinawataka wachimbaji wa madini kutenga asilimia 20 ya uzalishaji wao kwa ajili ya kuiuza katika masoko ya ndani ikiwemo kuiuzia Benki Kuu ya Tanzania, ambayo imepewa haki ya kwanza kisheria ya ununuzi wa dhahabu.

‘‘Sambamba na hiyo, hatua hii itaiwezesha Benki Kuu kupata vyanzo vya uhakika katika kufanikisha programu yake ya ununuzi wa dhahabu na itasaidia viwanda vya ndani vya usafishaji wa dhahabu kufikia malengo ya kupata ithibati ya kimataifa ya London Bullion Market Association (LBMA)’’, alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa mpango wa ununuzi wa dhahabu ni dhamira ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, kuongeza mchango wa madini katika pato la Taifa, pamoja na kuongeza thamani ya madini nchini ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za madini.

‘‘Hadi leo Benki Kuu ya Tanzania, imenunua tani 5 za dhahabu sawa na dola za Marekani milioni 554 na kupitiliza malengo yake ya kununua dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 350, Hatua hii ni kubwa na ya kihistoria nchini kwetu, kwa kuwa itatuhakikishia kuwa na dhahabu ya kutosha hapa nchini kwa ajili ya kusafishwa na viwanda vilivyopo hapa nchini, lakini pia kuipa Benki Kuu ya Tanzania, ambayo imeamua kununua na kutunza dhahabu kama sehemu ya fedha za kigeni’’, alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba.

Alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa kanuni hiyo mpya, Benki Kuu imeweza kuongeza kwa kasi kiwango cha dhahabu inayonunua kutoka katika soko la ndani na hivyo matarajio ni kwamba itaweza kufikia malengo yake ya kununua tani 6 za dhahabu kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ili kutunisha akiba ya fedha za kigeni.

‘‘Nitoe wito wa Serikali na wadau wote katika jambo hili kuhakikisha kwamba mkakati huu wa Serikali kununua dhahabu unakuwa endelevu. Lengo ni kwamba kama taifa tunakuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni katika dhahabu, kwani kwa muda mrefu sasa imedhihirika kwamba bei ya dhahabu imekuwa ni nzuri na inayozidi kupanda mwaka hadi mwaka’’, alisema Mhe. Nchemba.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde alisema sekta hiyo imeongeza mchango wake kwa pato la Taifa kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024/25.

Alifafanua kuwa sekta ya madini ilikuwa inachangia kiasi cha Sh. bilioni 162 mwaka mzima katika Mfuko Mkuu wa Serikali lakini baada ya marekebisho ya Sheria kwa sasa inachangia kiasi cha Sh. bilioni 753 wakati lengo ni kufikia sh. trilioni moja, lengo ambalo alisema litafikiwa.

“Hiki ni kiasi kikubwa kuwahi kutokea na hii inatokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye anatuongoza vema katika nchi yetu, kuhakikisha madini yanaongezwa thamani na kuchangia katika Uchumi wa nchi yetu,’’alisema Mhe. Mavunde.

Awali Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, alibainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania ilianza rasmi Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu nchini katika mwaka wa fedha 2022/23 kama sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Taifa ya kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje kama chanzo kikuu cha akiba ya fedha za kigeni na hivyo kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea kifedha.

‘‘Hadi kufikia tarehe 13 Juni 2025, Benki Kuu imefanikiwa kununua kilo 5,022.85 za dhahabu safi, zenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani milioni 554.28, Ikiwa imezidi lengo lake la mwaka la kuongeza akiba ya fedha za kigeni kiasi cha dola za Kimarekani 350 million kwa 2024/25’’, alifafanua Bw. Tutuba.

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo, Benki Kuu imelenga kuongeza kiwango cha dhahabu kinachotumika kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uhimilivu wa akiba ya fedha za kigeni nchini.

Kwa upande wao kampuni za madini zilizosaini mikataba hiyo za Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), zimeishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya madini nchini na kuahidi kuwa mikataba hiyo itafungua fursa zaidi katika sekta ya madini.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment