Alhajj Hemed ameyasema hayo wakati alipokuwa akisalimiana na waumini wa dini hiyo kwenye msikiti wa Nour Abswar uliopo Kiembe Samaki mara baada ya kumalizika kwa sala ya Ijumaa.
Amesema kushukuru neema mbalimbali ambazo Mwenyezi Mungu amewapa waja wake wakiwemo wa Zanzibar, ni jambo la muhimu sana ambapo miongoni mwa neema hizo wengine hakuwajaalia.
Alhajj Hemed alitoa mfano sekta ya elimu, amesema kunashuhudiwa kuongezekeka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha sita, jambo ambalo ni neema kubwa kwa Zanzibar.
Amesema hatua ya viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na maono ya kuimarisha miundombinu mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, imewezesha kufikiwa kwa neema hiyo ya kuongezeka kwa ufaulu.
Mhe. Hemed amesema kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa skuli za Zanzibar kunazidi kutoa matumaini ya ongezeko la wataalamu wazawa wa fani mbali mbali ambao watakuja sehemu muhimu kusaidia maendeleo ya nchi yao.
Akizungumzia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, Alhajj Hemed amesema serikali imejipanga katika kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa salama na amani.
Amesema serikali haitamfumbia macho wala kumuonea muhali mtu yoyote atakae jaribu kwa njia yoyote kusababisha uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi huo.
Amewataka viongozi wa kisiasa na wananchi kuhubiri amani, utulivu, umoja na mshikamano pamoja na mambo yote yatakayosaidia kuijenga Zanzibar na ni muhimu kukumbuka kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na wazanzibari wote ni ndugu.
Akitoa hotuba katika sala ya Ijuma, Sheikh Said Ameir amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kuamrishana mema na kukatazana mabaya, hatua ambayo itawawezesha kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Sheikh Said amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuachana na matendo maovu na kuwa na maazimio ya kweli kwenye nafsi zako katika kufanya amali njema zenye manufaa baada ya maisha ya duniani.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 11.07.2025
No comments:
Post a Comment