Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizindua mfumo wa anuwani za makazi Zanzibar katika hafla ya utambulisho wa Mfumo huo iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.Imetolewa na Kitengo cha Habari.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema mfumo wa anwani za makazi ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha ulinzi na usalama na ufikishaji wa huduma kwa wananchi.
Ameyasema hayo katika hafla ya utambulisho wa matumizi ya mfumo huo Zanzibar, iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni.
Amesema mfumo huo utasaidia kutambua na kufikia maeneo ya karibu ili kujipatia huduma kama vile vituo vya afya, maduka ya bidhaa, maeneo ya ibada na mengine muhimu.
Mhe. Hemed amesema tukio hilo linatoa nafasi ya kuanza rasmi utoaji wa barua za utambulisho wa makazi kwa njia ya kidijitali ambapo mwananchi popote alipo atafikiwa.
Amewahamasisha wananchi na wageni wanaoingia nchini kutumia mfumo huo ambao utarahisisha upatikanaji wa huduma.
Amewataka wananchi kuendelea kutunza na kuilinda nguzo za majina ya barabara zilizowekwa na serikali kusaidia wananchi kutambua mitaa yao, dhidi ya watu wenye tabia ya kung’oa nguzo hizo.
Ameiagiza Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, kusimamia utekelezaji wa matumizi ya mfumo huo katika ngazi mbali mbali na kuhakikisha waatendaji wa wadi na masheha wanaendelea kusajili, kuhakiki na kuimarisha taarifa anwani makazi.
Sambamba na hayo, ameagiza kujengewa uwezo watendaji wote wanaoshughulikia mfumo huo na kuitaka ZANROAD kwa kushirikiana na halmashauri zote kuweka miundombinu ya anwani za makazi kwenye mitaa au barabara ambazo wana dhamana ya kuzihudumia.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Massoud Ali Mohammed, amesema ofisi yake inatambua umuhimu wa mfumo wa anuwani za makazi ambao unatumika kama daftari la utambuzu wa makazi.
Amesema katika mwelekeo wa serikali ya kutoa huduma kwa njia ya kidijitali, ofisi yake itawapatia mafunzo watendaji wote wanaoshughulikia mfumo huo wakiwemo masheha na wasaidizi wao ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Massoud wizara itaendelea kuimarisha mfumo huo na kutoa elimu kwa wananchi ili kila mmoja atambue umuhimu wa matumizi wa anwani za makazi katika maisha ya kila siku.
Waziri wa Mwasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania,Jerry William Silaa, amesema taarifa za anwani za makaazi zinatumika katika kupanga mambo mbali mbali ikiwemo kufikisha huduma nyumbani na kuomba mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Amefahamisha kuwa serikali inapotekeleza uchumi wa kidijitali ni lazima kuwepo kwa mfumo huo ambao hurahisisha upatikanaji wa taarifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Habiba Hassan Omar, amesema wizara inaendelea kuwajengea uwezo masheha kwa kuwapatia vishikwambi vitakavyotumika kutolea barua kwa wananchi wanaofika kupatiwa huduma hiyo.
Dk. Habiba amesema dhamira yao ni kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa anwani za makazi kwa kutambua namba zao za nyumba, mitaa na sehemu zote muhimu zinazotolewa huduma za kijamii na kiuchumi ili kutanua upatikanaji huduma.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR ) Tarehe 16.08.2025
No comments:
Post a Comment