Menu

Thursday, August 28, 2025

UTUNZAJI SAHIHI WA NYARAKA NA KUMBUKUMBU NI MSINGI WA TAIFA IMARA-MAJALIWA

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akizungumza na wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) wakati alipofungua Mkutano wa 13 wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam Agosti 27, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

UTUNZAJI sahihi wa nyaraka na kumbukumbu ni uti wa mgongo wa uwajibikaji, historia, na utawala bora kwani bila masjala madhubuti, Taifa letu lingeweza kukabiliwa na changamoto kubwa za upotevu wa taarifa, ucheleweshaji wa maamuzi, na hatimaye kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.

 

Hivyo, Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania Tanzania (TRAMPA) kinabeba dhamana kubwa kwa Taifa letu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nyaraka na kumbukumbu zote muhimu za Serikali na taasisi binafsi, zinatunzwa kitaalamu, zinahifadhiwa kwa usalama, na zinapatikana kwa urahisi zinapohitajika.

 

Katika Mkutano Mkuu wa 13 wa TRAMPA, uliofanyika Agosti 27, 2025 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisisitiza umuhimu huu. Alibainisha kuwa chama hicho kinalenga kukuza utaalamu na weledi wa usimamizi wa nyaraka kwa kuhimiza utoaji wa mafunzo na miongozo ya kitaalamu.

 

Alisema mafunzo na miongozo ya kitaalamu inatolewa ili kuhakikisha nyaraka zote zinatunzwa kwa viwango vya juu vya usiri, usahihi, na usalama. “Aidha, Chama kimekuwa mstari wa mbele katika kuchochea uwajibikaji na utawala bora.”

 

“…kwa mantiki hiyo, TRAMPA inabaki kuwa injini muhimu katika kuhakikisha Taifa letu linaendelea na safari yake ya maendeleo kwa kuzingatia uwazi, weledi na uadilifu katika utunzaji wa taarifa.”

 

Hivyo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa watunza kumbukumbu wote nchini kuzingatia maadili ya kazi, kudumisha uadilifu na kulinda usiri wa taarifa zote zinazohifadhiwa kwani taarifa hizo ni nyenzo muhimu ya usalama wa Taifa na maendeleo ya nchi.

Mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu isemayo: “Matumizi ya Ofisi Mtandao ni Chachu ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Ustawi wa Taifa Letu.”

 

Waziri Mkuu alisema kaulimbiu hiyo imebeba maono makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mapinduzi ya kidijitali yanayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi, uwajibikaji wa taasisi, na uwazi katika shughuli zote za umma.

 

Alisema kupitia kaulimbiu hiyo watunza kumbukumbu hao wanakumbushwa kuhakikisha mifumo katika taasisi zote za umma inasomana, na kutoa huduma kwa pamoja ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma kwa haraka na usahihi.

 

Waziri Mkuu aliongeza kuwa kaulimbiu hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Taifa linaweka msisitizo mkubwa katika matumizi ya Ofisi Mtandao (e-Office) na mifumo ya kidijitali inayounganishwa serikalini.

 

“Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya TEHAMA, ikiwemo mifumo ya malipo, utunzaji kumbukumbu, na ufuatiliaji wa utendaji kazi wa watumishi, ili kuimarisha uwajibikaji na kuziba mianya ya rushwa.”

 

Alisema Serikali inatarajia kuwa TRAMPA itaendelea kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika masjala, nyaraka na kumbukumbu za Taifa ili kuhakikisha nchi inasonga mbele kwa kasi kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika na duniani kote.

 

Katia hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali pamoja na kuendeleza masijala za kisasa.

 

Alisema mafanikio hayo yamejitokeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji mkubwa katika TEHAMA, ambapo kupitia mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), Wizara, Idara, Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali zimewezeshwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa kumbukumbu.

 

Pia, Waziri Mkuu alisema uwekezaji huo umeongeza uwazi na kupunguza ucheleweshaji wa huduma. Vilevile, miradi mikubwa kama Tanzania Data Lab na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Nyaraka za Serikali (e-GA Records System) imeimarisha kwa kiasi kikubwa kasi ya utoaji huduma kwa wananchi na kuongeza uwajibikaji wa taasisi za umma.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TRAMPA Taifa, Devota Mrope alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta mbalimbali iliwemo katika kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka.

 

“Rais Dkt. Samia amekuwa mwana TRAMPA namba moja, amepigania maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo sisi  mwana TRAMPA, ametoa ajira nyingi katika kipindi kifupi ikiwemo kwa  wanataaluma wa kada hii ya Menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka, amefanyia kazi changamoto zetu kwa kiasi kikubwa.”

 

Mwenyekiti huyo alisema mapinduzi makubwa ya kidigitali yaliyofanyika nchini ikiwemo matumizi ya ofisi mtandao ni chachu ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwani yapo mafanikio ya wazi katika idara, wizara na ofisi za Serikali ambazo zimejikita katika matumizi ya ofisi mtandao katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

 

Alisema matumizi ya Serikali mtandao yamesaidia kurahisisha michakato ya utendaji kazi katika Taasisi za Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi ili kufikia dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 baada ya kuongeza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, uwazi katika utendaji kazi na uadilifu mahala pa kazi.

 

“Matumizi ya Serikali mtandao yanapunguza gharama za uendeshaji ofisi Serikali na pamoja na kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa Taasisi za Umma, kwa kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ya haraka, yenye uhakika na salama ndani na nje ya Taasisi za Serikali.”

 

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejiementi ya Utumishi wa Umma ma Utawala Bora, George Simbachawene alisema kuwa Serikali imeeendelea kutoa ajira kwa watumishi wa umma wakiwamo watunza kumbukumbu. “Kada hii tu ajira mpya zilizotolewa ni 965 waliopandishwa madaraja ni 1237, ikiwemo kuwabadilishia kazi watumishi 59 (Recategorization) pamoja na kulipa malimbikizo ya shilingi bilioni 200”.

 

Alisema kuwa Serikali inatambua mchango kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka  katika ustawi wa utumishi wa umma na wakati wote itaendelea kutoa ushikiano kwa kada hiyo ili kuendelea kufanikisha masuala mbalimbali ya kiutumishi.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora   wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haroun Ali Suleiman aliwapongeza wanachama wa chama hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya utunzaji wa siri za ofisi kwa maslahi ya Taifa. “Pamoja na hili ninawapongeza sana kwa uamuzi wenu mzuri wa ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa”.

 

Alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa kada hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajenga jengo kubwa na la kisasa la utunzaji kumbukumbu ambalo litazinduliwa hivi karibuni. “Pia Serikali kwasasa inajenga majengo mapya ya kisasa na katika hili tunazingatia uwepo wa ofisi nzuri za watunza kumbukumbu.” 

 

Mkutano wa 13 wa TRAMPA umeweka wazi kuwa utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu si jukumu la kawaida, bali ni msingi wa uhai wa Taifa. Serikali na wadau wameonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha mifumo ya kisasa, kukuza weledi na kutumia teknolojia kama kichocheo cha maendeleo.

 

Kwa msingi huo, nyaraka na kumbukumbu bora zinabaki kuwa injini ya utawala bora, usalama wa Taifa, na nguzo ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

 

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

ALHAMISI, AGOSTI 28, 2025

No comments:

Post a Comment