Menu

Monday, September 8, 2025

KHADIJA MWAGO WA CHAUMA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE MBAGALA

Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.

Mgombea ubunge wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hadija Mwago, kuzindua rasmi kampeni zake katika jimbo la Mbagala, jijini Dar es Salaam huku akiahidi kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo.

Pia,ameahidi kama atapewa ridhaa atahakikisha anajenga kutuo cha afya kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto ili kuwasaidia wananwake kupunguza gharama pindi wanapokwenda kujifungua.

Hayo ameyaahidi Septemba 8,2025 Katika mkutano wake uliofanyika kiwanja cha Kwaserenge Mbagala, Mwago ameahidi kushirikiana na wananchi kujenga shule moja katika kila mtaa wa jimbo hilo, hatua ambayo amesema itapunguza msongamano wa wanafunzi na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora karibu na makazi yao.

“Wazazi hawatateseka tena kusafirisha watoto umbali mrefu kutafuta shule. Tukiweka shule kila mtaa, tutakuwa tumepunguza changamoto kubwa ya elimu na kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi,” amesema.

Sambamba na hayo Mgombea huyo ameahidi kuwekeza kwenye huduma za afya kwa kuongeza miundombinu ya zahanati na vituo vya afya, sambamba na kusimamia mifuko ya mikopo ya vijana na kinamama ili kukuza ajira na kujikwamua kiuchumi.

Aidha Mwago akizungumzia miundombinu ya barabara za ndani amesema pindi atakapopata ridhaa hata hakikisha barbara zote za ndani zinapotika wakati wote hata kama mvua zikinyeesha

Mwago amewataka wakazi wa Mbagala kuhakikisha wanachagua madiwani na Rais wa Chaumma, akisisitiza kuwa chama hicho ndicho mbadala wa kweli wa CCM, ambacho kimedumu madarakani kwa muda mrefu bila kuleta suluhisho za msingi za changamoto zinazowakabili wananchi.

“Wanambagala, kura zenu safari hii zinapaswa kuwa za ukombozi, tukipewa nafasi ya kuunda serikali, tutaleta maendeleo yanayomgusa kila mmoja wenu moja kwa moja,” amesisitiza Mwago.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa chama hicho Mkoa wa Dar es salaam na Mgombea ubunge jimbo la Chamazi HERMAN KILOLOMA amewataka wananchi kuhakikisha wanapiga kura ili chama hicho kikabadilishe mifumo iliyowowekwa na chama cha mapinduzi.

Pia ameongeza kuwa miundombinu ya mitaa ni mibovu hivyo wananchi watakapokipa ridhaa chama hicho kitakwenda kushughulikia miundombinu yote na kuondoa kero kwa wananchi pindi mvua zinaponyeesha.

“Haya yote yatafanikiwa ikiwa mtatuchagua CHAUMA msikubali kununuliwa kwa pesa ili mpige kura kuwachagua pesa hizo watazirudisha watakapokuwa madarakani kupitia miradi ya maendeleo”,Amesema….

Awali kabla ya kumkaribisha mgombea huyo,Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es salaam Husna Masoud amewataka vijana kuendelea na kampeni za nyumba kwa nyumba(mobile kampeni)ili kuhakisha wanakitafutia kura za kutosha chama hicho lakini kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya octoba 29,kwenda kupiga kura.

Naye, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kampeni na Uratibu wa Kitaifa wa Chaumma, Kangeta Ismail Kangeta, ametumia jukwaa hilo kuwaombea kura wagombea wote wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani huku akieleza sera kuu ya chama hicho ikiwa ni kujenga uchumi shirikikishi kati ya wananchi na serikali.

“Hatutaki serikali inayowaacha wananchi wake nyuma. Tunataka serikali ya wananchi, inayomilikiwa na wananchi, na itakayopigania masilahi ya wananchi,” amesema Kangeta.

Kwa kuzinduliwa kwa kampeni hizo, Chaumma sasa kimeingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Mbagala huku takribani vyama 13 vikiwemo CCM, CUF, ACT Wazalendo, NLD na Makini vikisimamisha wagombea kulisaka jimbo hilo la kusini mwa jiji la Dar es Salaam.







No comments:

Post a Comment