Menu

Friday, October 24, 2025

DKT JAKAYA KIKWETE AZURU MAKABURI YA MAKADA WENZAKE KABLA YA KUHITIMISHA KAMPENI ZA UCHAGUZI KATIKA MAJIMBO MATANO YA ZANZIBAR

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizuru kaburi la  Marehemu Mohamed Seif Khatib, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mara tu baada ya TANU na Afro Shirazi Part kuungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Uwanja wa Amaan Zanzibar mwaka 1977. 
Dkt. Kikwete akizuru kaburi la  Marehemu Ramadhani Abdallah Shaaban, mmoja wa viongozi wa awali wa chama hicho katika upya wake.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo amehitimisha rasmi kampeni za uchaguzi kwa majimbo matano ya Zanzibar, akianza kwa kuzuru makaburi ya makada wenzie wakongwe wa  CCM aliofanya nao kazi tangia anaigia kwenye siasa takriban miaka 48 iliyopita.

Dkt. Kikwete aliazuru makaburi ya  Marehemu Mohamed Seif Khatib, aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mara tu baada ya TANU na Afro Shirazi kuungana na kuunda CCM mwaka 1977, na la Marehemu Ramadhani Abdallah Shaaban, mmoja wa viongozi wa awali wa chama hicho katika upya wake.

Baadaye alihitimisha kampeni na majimbo ya Tunguu, Chwaka na Uzini katika Wilaya ya Kati, pamoja na majimbo ya Paje na Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja kwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Skuli ya Ghana jimbo la Uzini Wilaya ya Kati, Shehia ya Kiboje, Mkoa wa Kusini.

Rais huyo mstaafa amewashukuru wana CCM kwa kumchagua yeye kuwafungia rasmi kampeni na kuufanyia Mkutano huo katika jimbo la Uzini, mahala ambapo amesema ana uhusiano maalumu napo.

“Hapa ndipo kwao Marehemu Mohamed Seif Khatib, mtu ambaye katika uhai wake tulikuwa marafiki wa karibu kwa miaka mingi. Urafiki wetu ulianza mwaka 1977 mara baada ya mimi kuhamishiwa Zanzibar na kuja kufanya kazi Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui. Hii ilikuwa baada ya ASP na TANU kuungana na kuzaliwa CCM.

“Wakati ule Mohamed alikuwa anafanya kazi Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. Mimi nilikwenda pale kuomba kujifunza lugha ya kifaransa. Yeye rafiki yangu alikuwa Bingwa wa lugha ya Kiswahili, ndipo tulipokutana naye na tangu hapo basi tukawa marafiki.

“Mohamed na mimi tulianza safari yetu ya siasa wakati mmoja. Kwenye Mkutano Mkuu Mohamed Seif na mimi tukawa miongoni mwa vijana wa kwanza kuchaguliwa mwezi Oktoba 1982, wengine waliochaguliwa walikuwa Azan Aljabri, Daniel Ole Njoolay na Ditopile Mzuzuri.

“Novemba mwaka 1988, tuliteuliwa siku moja kuingia kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Ali Hassan Mwinyi, yeye akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, na mimi Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

“Nilipojitokeza kuomba uteuzi wa kugombea Urais kupitia tiketi ya CCM mwaka 1995 na 2005 aliniunga mkono. Nilipofanikiwa kkuchaguliwa kuwa Rais mwaka 2005 nilimjumuisha kwenye Baraza langu la Mawziri. Tumekuwa wote na hata nilipostaafu tuliendelea kushirikiana kwa mambo mbalimbali.

Hayo ni yangu mimi na swahiba yangu Mohamed Seif. Nimepata faraja kuona alipolala na pale alipolala rafiki yetu wa pamoja Marehemu Ramadhani Abdallah Shaaban. Tuendelee kuwaombea kwa Allah SWT makaburi yawe bustani za peponi na yasiwe mashimo ya motoni. Ameen.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment