6/recent/ticker-posts

CUF ITAWAPA MITAJI WAFANYABIASHARA --- MAALIM SEIF

Na Shaib Kifaya

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema akifanikiwa kuingia madarakani, atawawezesha wafanyabiashara Zanzibar.

Maalim Seif, alitoa kauli hiyo huko Fuoni kwenye mkutano wa kampeni wa kuomba ridhaa ya wananchi na kuwanadi wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa jimbo hilo.

Alisema ilani ya CUF ni kuwawezesha na kuwapa kila msaada wafanyabishara wa Zanzibar ikiwemo kuwapa mitaji ya kuendesha biashara hizo.

Katibu Mkuu huyo wa CUF, alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikwama njiani kwa kukosa mitaji ya kufanya biashara zao jambo ambalo litapatiwa ufumbuzi baada ya chama hicho kushinda kwenye uchaguzi mkuu.

Alisema wafanyabiashara ndoogo ndogo katika eneo la Darajani na Saateni hawatakimbizana na Askari wa Manispaa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu n chama hicho kufanikiwa kuingia madarakani.

"Matafanya biashara zenu bila ya wasi wasi, suala la kukimbizana n askari wa Manispaa litakoma nikiwa Rais wa nchi hii", alisema Maalim Seif.

Maalim Seif pia alizungumzia haja ya kuimarisha miundombinu pamoja na kuimarisha sekta za jamii ikiwemo elimu, maji, umeme, afya na kujenga viwanda ili kuweza kuwaondoshea ugumu wa maisha wananchi na vijana kuweza kupata ajira na kuondokana na utegemezi.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuyaenzi na kuyalinda maridhiano yaliyopo ambayo yamekuwa msingi wa amani miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha aliwasihi wanachama wa chama hicho kufika mapema kwenye vituo vya kupigia kura na baadae warudi majumbani kwa kusikiliza matokeo ya uchaguzi huo.

Post a Comment

0 Comments