Na Juma Masoud,
SERIKALI imeshauriwa kutoa taalumu kuhusu njia muafaka za kuepuka uvuvi haramu unaoendela kufanywa na wavuvi katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Mkoa wa Kusini Unguja Alhaj Haji Ameir, alipozunguma na mwandishi wa habari hizi jana.
Alisema kwa bahati mbaya tatizo la uvuvi haramu limechukua kasi kubwa takriban katika maeneo mengi ya Zanzibar, huku uchunguzi ukionesha kwamba sababu kubwa ya hali hiyo inasababishwa na wananchi hao
kutopewa taaluma ya kutosha kuhusu madhara ya uvuvi huo.
Alhaj Haji Ameir alisema tatizo la uvuvi haramu limekuwa jambo la mazoea na kuvitaka vyombo husika kuendelea kutoa taaluma hiyo na wakati huo huo kuwapatia njia mbadala wavuvi ili waachane na makosa
hayo.
Alisema yeye akiwa mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Kusini Unguja hapendelei kuona wavuvi wanaingia kwenye migogoro ya kulaumiwa kwa kuendesha uvuvi haramu hivyo, akapendekeza vyombo husika kusimamia mafunzo kama hayo ili wavuvi wenyewe wafahamu madhara ya aina hiyo ya uvuvi na faida zitokanazo na uvuvi salama.
Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza mizozo mbali mbali inayohusiana na uvuvi haramu na kusababisha mamia ya wavuvi kukamatwa, kunyang’anywa vifaa vya uvuvi na wegine kufunguliwa kesi mahakamani kwa kubainika kuendesha uvuvi wa aina hiyo.
Alisisitiza kuwepo taaluma na majadiliano kuhakikisha wavuvi wanaendelea na kazi yao kwa kufuata sheria kwani uvuvi ndio sehemu kubwa ya ajira yao
Katika hatua nyengine, takriban wavuvi 500 katika kijiji cha Jambiani waliamua kurejesha kadi zao za vyama wakipinga hatua ya kukamatwa na kunyang’anywa vifaa vya uvuvi, hali iliosababisha wengi wao kuchukua
uamuzi huo.
Katika siku za karibuni wavuvi wa Mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja walikamatwa kwa tuhuma hizo na kesi zao bado ziko mahakamani.
0 Comments