6/recent/ticker-posts

Ofisi ya Rais Yaanika Mafanikio ya Wizara Julai - Disemba 2011

Na Ramadhan Ali-Maelezo

WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika mwaka wa fedha 2011/2012 imelenga kutekeleza mipango iliyowekwa katika dira ya 2020, maendeleo ya milenia, kukuza uchumi na kupunguza umaskini pamoja na kutekeleza ilani ya ccm ya 2010-2015.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi Kiwajuni kuhusu majukumu, malengo, mafanikio pamoja na mikakati ya wizara hiyo kwa kipindi cha Julai mpaka Disemba 2011, waziri wa wizara hiyo Mh. Mwinyihaji Makame amesema kipaumbele kimewekwa katika kuendeleza umoja wa kitaifa, utoaji huduma na kuwashajiisha wazanzibari wanaoishi nje kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Amesema Wizara hiyo imeweza kutekeleza malengo yake iliyojiwekea ya nusu mwaka kama ilivyojipangia, ikiwemo kukuza mashirikiano ya kikanda na kimataifa, kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

Hata hivyo Mh. Mwinyihaji Makame amesema pamoja na mafanikio hayo wizara inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uhaba wa vitendea kazi na watendaji wenye taaluma kwa baadhi ya kada na ukosefu wa nafasi za kufanyia kazi pamoja mlundikano wa mahabusu magerezani.

Amesema Wizara ya Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imepanga mikakati mbali mbali katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi wapya kwa mujibu wa mahitaji ya wataalamu hasa katika mikoa, wilaya na halmashauri ili kuongeza ufanisi.

Dk. Mwinyihaji amefanya mkutano huo na waandishi wa habari ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais Shein kwa Mawaziri kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mafanikio na changamoto za utekelezaji katika Wizara zao


Post a Comment

0 Comments