Na Thabit Jaha, Zanzibar.

Chama cha Mapinduzi(CCM) kimesema Muungano hautavunjwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu kwani Jumuiya hiyo haina mamlaka ya kuwaamulia Watanzania hatma na mustakabali wao.
Onyo hilo limetolewa na Jumuiya tatu za CCM katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa mabata Zanzibar ambapo iliweka bayana msimamo wa Chama hicho kulinda Muungano na Mapinduzi kwa gharama yoyote.

“Sisi tunawaambia Muungano hautavunjika kwa kisingizio cha katiba mpya,katiba mpya ni sehemu tu ya mabadiliko ya kukuza demokrasia ya utawala…CCM ikiwa zao la ASP na TANU tunawajibu wa kutetea historia yetu ya umoja na mshikamano” Alisema Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ramadhan Abdallah Ali


Alisema kumejitokeza kikundi cha watu wanaojificha kwenye mwamvuli wa Jumuiya ya kidini kuandesha kampeni chafu za kusambaratisha Taifa la Tanzania kwa kutumia mpango mkakati wa kutoa elimu ya uraia Visiwani Zanzibar na kushangazwa na vyombo vya Dola kuwafumbia macho watu hao.

“Vyombo vya Dola vinakaa kimya,viongozi wa Kitaifa wanatukanwa na kudhalilishwa na kikundi hichi, haiwezekani watu wanachochea uasi dhidi ya Jamhuri,lakini hakuna hatua zinazochukuliwa…CCM tunasema muda wa kuwavumilia umekwisha” Alionya Mjumbe huyo.

Alisema kwamba wanaopinga na kutaka kuvunja Muungano wa Tanzania pia wana lengo na mipango maalum ya kusambaratisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ambayo yaliongozwa na ASP .

“Kwa kweli tusifanye mchezo na uchochezi unaofanywa na watu hao, vikundi kama hivi ndio vilianzisha vurugu katika Mataifa mbalimbali,leo mnasikia kuna Al shabab,Boko- haram,Fisi na wengineo wote hao kabla walijificha kwenye mwamvuli wa dini,hawa wa Zanzibar tumashawabaini, tuwakatae” Alisisitiza.
Mkutano huo umefanyika huku kukiwa na kundi lililoanzisha kampeni ya hadharani kushawishi wananchi kukataa Muungano kwa madai kwamba haujaleta faida kwa Wazanzibari.

Mbali na udini, pia kikundi hicho haikijitofautisha na vyama hasimu vilivyokuwa vikipinga Muungano ambapo matamshi yao, vitendo na muenekano wao hauna tofauti na wapinga mapinduzi.

Katibu huyo mstaafu wa CCM Mkoa Mjini Magharibi amesisitiza kuwa Mapinduzi ya 1964 ndiyo yaliowaletea heshima na kutambuliwa kwa utu wao waafrika wanyonge waliokuwa wakibaguliwa na kutumikishwa.

“Hakuna mjinga yeyote hapa Zanzibar asiejua kuwa mpango wao si kueneza dini ila ni kutaka kusambaratisha Mapinduzi,wao wanaelewa fika kuwa Muungano huu hautavunjika milele kwasababu hawakuunda wao na wala hawatambui madhumuni ya nchi mbili hizi kuunganishwa ”Alisema Ali

Ali aliwakumbusha wananchi utawala wa Kifalme wa Oman waliikalia Zanzibar kwa miaka 132 kwa kulindwa na Uingereza wakichota rasilimali ,kuwatumikisha na kuwabagua wananchi bila ya kufanyika kura ya maoni ili kujua wananchi wangapi wanautaka ukoloni au wanaupinga.

Alitoa mfano kuwa tangu kufuzu kwa Mapinduzi,Mfalme na aila yake, wapinga mapinduzi walijaribu kutaka kuyaondoa mapinduzi ambapo jaribio kubwa ni lile la kumuua Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,marehemu Abeid Amani Karume.

Alisema wana CCM na wazalendo wengine hususan wanyonge wa Zanzibar wanajua kuwa wale waliopinduliwa hawakupenda kuondoshwa na hadi sasa bado wanaota na kutamani kurejea kushika utawala.

“Uamsho msijifiche nyuma ya kivuli cha dini,uislam ni dini adhim na tukufu,hakuna hata dini yoyote inayoelezea uvunjifu wa amani kwa kuchochea utengano miongoni mwa jamii, acheni kujifanya mnaeneza dini wakati mnafanya siasa” Alionya.

Akizundua Tume ya Katiba,Rais Jakaya Kikwete alisisitiza kwamba katiba mpya haitavunja Muungano na kuwaonya watu wanaochochea suala hilo kuacha mara moja.