Na Madina Issa
KATIKA mchezo wa kirafiki kuadhimisha ‘Wiki ya Maji Duniani’, timu ya Paje Stars iliwachapa bila soni maofisa na mainjinia wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) mabao 3-0.
Pambano hilo lililochezwa katika uwanja wa Paje, nyavu za ZAWA zilianza kuhujumiwa mnamo dakika ya 15 kwa bao lililofungwa na Lucas Makaranga, kabla Aduli Ndame kuongeza la pili katika dakika ya 20.
Mabao hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko, na wenyeji wakarudi kipindi cha pili kwa kasi zaidi na kufanikiwa kuandika bao la tatu katika dakika ya 55 kupitia kwa Mbarak ‘Zidane’.
Mbali na mechi hiyo, sherehe hizo pia zilipambwa na resi za mbatata zilizotawaliwa na kijana wa Paje, Safia Pandu, na mchezo wa kutembea kwenye kamba ambapo mchezaji wa ZAWA Khamis Abdallah aliibuka kidedea.
Michezo mingine iliyorindima kijijini hapo ni kufukuza kuku, kula maandazi, mbio mita 100 na resi za magunia, ambapo washindi na wafanyakazi mbalimbali wa Mamlaka ya Maji Zanzibar walitunukiwa zawadi.
0 Comments