Na Salum Vuai, Maelezo
KUWEPO kwa ongezeko la dawa za uhakika za kutibu magonjwa mbalimbali, kutasaidia kuongeza ushindani na kupunguza uhalifu wa dawa bandia katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.Mkurugenzi wa Wizara ya Afya, Dk. Malik Abdallah Juma, alisema bado nchi za ukanda huo zinakabiliwa na changamoto ya kuwa na mfumo usio salama katika upatikanaji wa dawa za magonjwa ya kawaida kwa kiwango kikubwa hali inayochangia hatari ya maisha ya wananchi.
Akifungua mkutano wa mpango wa pamoja wa kusimamia usalama wa dawa kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki uliofanyika jana katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya manispaa ya Zanzibar, Dk. Malik aliwataka washirki wa mkutano huo kuandaa sera ya pamoja katika kusimamia dawa hasa za binadamu, ili kuwahakikishia wananchi wa nchi zao usalama wa dawa na afya zao.
Alieleza kuwa,kuwepo kwa utaratibu huo utasaidia kupunguza gharama kwa serikali, mashirika ya kimataifa na jamii kwa ujumla, sambamba na ongezeko la soko la bidhaa za dawa.
Aidha alifahamisha kuwa, mpango huo utaharakisha uandaaji wa sera na sheria za kuhakikisha usalama wa dawa, na hivyo kuleta ufanisi katika usimamizi wa kwa nchi wanachama za ukanda huo.
Hata hivyo, aliwaomba wafadhili kuendelea kusaidia harakati za kuimarisha usalama na usimamizi wa dawa, kwani bado nchi za Afrika Mashariki zinakabiliwa na ukosefu wa wataalamu na fedha.
“Hali hiyo inasababisha nchi hizo kuendelea kutegemea misaada ya wahisani, huku wanaofanya biashara ya dawa wakiendelea kuziuza kwa bei ya juu”, alisema.
Alisema kwa sasa Zanzibar inaendelea na mpango wa kuanzisha mamlaka ya dawa na kupitia sheria ya chakula, dawa na vipodozi ya mwaka 2006, ili iende sambamba na mkakati wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alieleza matumaini yake kuwa, mkutano huo wa siku mbili unaomalizika leo, utakuja na muongozo na mapendekezo mazuri juu ya namna ya kuimarisha na kuweka utaratibu muafaka wa usimamizi wa dawa.
Kwa hivyo, amewataka washiriki wa mkutano huo kutambua kuwa kazi waliyo nayo inagusa ustawi na maisha wa watu wa nchi zao.
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Dawa, Chakula na Vipodozi Zanzibar, Dk. Burhan Simai, alisema mkutano huo ni hatua muhimu katika kupata mawazo juu ya kudhibiti uhalifu wa dawa, ambao mara nyengine kuchangia kuingizwa kwa dawa bandia katika soko.
Naye mjumbe wa Kamati ya Mpango wa pamoja kusimamia dawa Afrika Mashariki Jane Mashingia Sudi, alisema jumuiya hiyo inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha huduma bora za dawa na usalama wa chakula kwa watu wake.
0 Comments