Na Mwandishi wetu, Oman
OMAN imeahidi kuliimarisha
Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kwa kulipatia vifaa vitakavyoliwezesha
kukusanya na kurusha matangazo yake na kuonekana vyema katika nchi za Mashariki
ya Kati.
Ahadi hiyo imetolewa mjini
Muscat, Oman na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Redio na Televisheni za Umma wa Oman,
Dk.Abdullah Bin Nasser Al Harrasi, wakati akizungumza na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar, Mhe. Said Ali Mbarouk akiwa katika
siku ya tatu ya ziara yake nchini humo.
Alisema mamlaka yake ina dhima
kuimarisha uwezo wa matangazo ya shirika hilo na kuonekana vyema Oman na
kwengineko na hivyo iko tayari kulipatia vifaa vya kurushia matangazo kwa njia
ya satellite na matangazo ya moja kwa
moja kwenye matukio nje ya studio.
Alisema hatua hiyo itazidisha
kuimarisha uhusiano uliopo kwa vile itawawezesha wananchi wa Oman kuangalia
vipindi vinavyorushwa na ZBC kwa wepesi zaidi kama ilivyo kwa matangazo ya
redio na televisheni ya Oman yanavyopatikana Zanzibar.
Alisema kwa kuanzia kutakuwa na
utaratibu wa kubadilishana mafundi na
watayarishaji vipindi ili kuweka misingi ya kuandaa kwa pamoja vipindi vitakavyotumia
lugha ya Kiswahili na Kiarabu na
kuwawezesha wananchi wa Oman na Afrika ya Mashariki kwa ujumla kufaidika
na matangazo ya vituo hivyo.
Akitoa shukrani kwa mamlaka
hiyo, Waziri Mbarouk, alipongeza hatua hiyo inayokusudiwa kuchukuliwa na Oman
na kusema sio tu itawawezesha wananchi wa pande hizo mbili kuendelea kuelewana
zaidi na kupatiwa taarifa juu ya masuala mbali mbali lakini pia itasaidia
kukuza na kuinua kiwango cha utalii katika nchi zote mbili.
Waziri Mbarouk yuko Oman kwa
ziara ya siku nne kutembelea vyombo vya habari, utamaduni na utalii na michezo
kwa mwaliko wa serikali ya Oman kwa madhumuni ya kutafuta njia za kuimarisha
uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
0 Comments