STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
27.8.2014
UFARANSA imeahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini
mwake kupitia makampuni yake makubwa ya kitalii yaliopo nchini humo sambamba na
kuendelea kuziunga mkono sekta nyengine za maendeleo za hapa nchini.
Balozi mpya wa
Ufaranza nchini Tanzania Mhe. Malika Berak aliyasema hayo leo wakati alipofanya
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwemyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo, Balozi Berak alimuhakikishia Dk. Shein kuwa afisi yake itachukua juhudi
za makusudi katika kuhakikisha Makampuni makubwa yanayofanya kazi za kitalii
yaliopo nchini Ufaransa pia, yanafanya kazi zake na hapa Zanzibar.
Alisema kuwa
kutokana na Ufaransa kupiga hatua kubwa katika sekta ya Utalii sambamba na kuwa
na watalii wengi wanaotembelea nchi mbali mbali ikiwemo Zanzibar ni jambo la busara
kwa makampuni hayo kuongeza juhudi na kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar
katika sekta ya utalii
Balozi huyo wa
Ufaransa alisema kuwa kwa vile Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya
kitalii pamoja na mikakati madhubuti
iliyowekwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta
hiyo hivyo nchi hiyo nayo iko tayari kuziunga mkono juhudi hizo.
Aidha, Balozi
Berak alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano wake na
kuimarisha uhusiano uliopo kwa kushirikiana pamoja katika kuinua sekta mbali
mbali za maendeleo na kiuchumi ikiwa ni pamoja na ushirikiano kwenye sekta ya
elimu, utamaduni na nyenginezo.
Nae Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimpongeza
Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini Tanzania na kumueleza kuwa Zanzibar na
Ufaransa zina uhusiano wa muda mrefu tokea karne ya 19.
Dk. Shein alisema
kuwa azma hiyo ya Ufaransa ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuitangaza na kuiimarisha sekta ya utalii nchini mwake
itasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi hasa ikizingatiwa kuwa Ufaransa ni miongoni
mwa nchi ambayo watalii wake wengi huitembelea Zanzibar.
Dk. Shein alisema
kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuimarisha sekta
za maendeleo mikakati kabambe imewekwa na serikali anayoiongoza katika
kuhakikisha huduma zote za kitalii zinaimarika ikiwa ni pamoja na uwekezaji na
hali ya usalama katika sekta hiyo.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo wa Ufaransa kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo na kusisitiza kuwa ipo haja ya
kuendelezwa kupitia sekta ya elimu kwa
wanafunzi kutoka Ufaransa kuja kusoma kiswahili hapa Zanzibar na wale wa
Zanzibar kwenda nchini humo kujifunza.
Akitoa historia
ya uhusiano kati ya pande mbili hizo, Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa nchi
za mwanzo kuweka Ubalozi wao mdogo hapa Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya
Januari 12,1964 ni Ufaransa ambapo alimueleza balozi huyo haja ya kuwepo huduma hizo kwa kuanzisha Ubalozi mdogo au huduma
za Balozi wa heshima ili ubalozi huo
uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi
zaidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alifanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Ali Said Siwa ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga
Rais na kutoa shukrani zake kwa Dk. Shein kwa kumpa moyo na kumuamini katika
utendaji wake wa kazi.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake alimpongeza Balozi huyo Mteule kwa kuteuliwa kuwa Balozi nchini
Rwanda na kumueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania ikiwemo
Zanzibar na Rwanda na kumueleza haja ya kuimarishwa na kuendelezwa.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Rwanda zina uhusiano na
ushirikiano wa muda mrefu katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu, utalii wa ndani huku akisisitiza haja
kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar.
Wakati huo huo, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia
salamu za pongezi Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa kuadhimisha siku ya taifa
ya nchi hiyo.
Katika salamu
zake hizo Dk. Shein amesema yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wanayo furaha
katika kuadhimisha siku hii ya Taifa ya nchi hiyo na kumpongeza Mheshimiwa
Erdogan kwa kuiongoza vyema Uturuki sambamba na kuimarisha umoja na kuleta
ustawi wa wananchi wake.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments