STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
19.1.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha uchumi wake unazidi kuimarika ikiwa ni
pamoja na kutafuta mbinu bora na matokeo yenye ustawi katika mageuzi ya
kiuchumi.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano uliojadili juu ya matokeo stawi katika
kukuza uchumi, uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuwashirikisha viongozi wa
ngazi za juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwemo Mawaziri, Manaibu
Waziri pamoja na Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wengine wa
Serikali.
Makamo wa Kwaza
wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Makamu wa Pili wa Rais
Balozi Seif Idd nao walishiriki ambapo ujumbe wa Wataalamu kutoka Malaysia na
Tanzania Bara walitoa mada mbalim mbali na baadae ziliweza kujadiliwa na
viongozi hao walioshiriki katika mkutano huo.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua
juhudi za makusudi katika kuhakikisha ustawi na mabadiliko ya haraka ya
kiuchumi yanafanyika hapa nchini hatua ambayo imeanza kuonesha matumaini na
kuleta mwanga katika ukuaji wa uchumi huo.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa wataalamu kutoka Malaysia akiwemo
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia, ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi
wa Utafutaji ufumbuzi wa matatizo kwa njia za vikao vya wataalamu mbali mbali (Maabara)
ya Malaysia ( PEMANDU) Dk. Idris Jala ambaye ni miongoni mwa watoa mada katika
mkutano huo.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazithamini na kutoa pongezi kwa
mtaalamu huyo pamoja na ujumbe wake kutoka nchini Malaysia kwa kuja Zanzibar na
kutoa mafunzo hayo sambamba na kuweza kubadilishana uzoefu juu ya matokeo
ustawi na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na utekelezaji wake.
“Tumevutiwa na
juhudi zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Malaysia katika programu
zake za matokea makubwa na ya haraka katika kukuza uchumi wake.. aidha, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Dk.
Idris Jala kwa matokeo na mwelekeo mzuri wa kitengo anachokiongoza cha PEMANDU ”,alisema
Dk. Shein..
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inazipongeza hatua inazozichukua Malaysia katika kuisaidia Zanzibar kwa kuipa
nafasi za masomo nchini humo katika kada mbali mbali zikiwemo programu za
kiuchumi.
Alieleza kuwa
nafasi hizo za mafunzo inazozipata Zanzibar ni muhimu na zimekuwa zikisaidia
katika kufikia lengo ililojiwekea katika utekelezaji wa masuala ya kiuchumi na
kukuza maendeleo.
Dk. Shein alisema
kuwa mnamo mwaka 2014 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitayarisha mbinu za kupata matokea ya ustawi na ya haraka katika
suala zima la kukuza uchumi wake.
Alieleza kuwa
lengo kubwa la utekelezaji wa ustawi huo ni kuimarisha programu kuu za
maendeleo katika sekta zilizopewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa
Dira ya 2020, Malengo ya Milenia pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini Zanzibar, Awamu ya Pili (MKUZA II).
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa ni bahati ya pekee kupata timu ya wataalamu kutoka
nchini Malaysia kuja Zanzibar kwa lengo la kukaa pamoja na kutoa elimu juu ya
hatua za kiuchumi zilizoipa mafanikio nchi hiyo pamoja na kubadilishana uzoefu na wataalamu na
viongozi wa hapa nchini.
“Ninaimani kubwa
kwamba elimu tutakayoipata katika mkutano wetu huu wa leo itatupa mwelekeo
mzuri katika azma yetu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini mwetu...Zanzibar
imo katika kujifunza kutoka Tanzania Bara njia zilizotumika katika kufanikisha
upatikanaji wa matokeo makubwa ya haraka ya kiuchumi‘Big Fast Result’ambapo
imeanza kuona matokeo yake”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa mambo matatu makubwa yakiwa na malengo yake yalipitishwa katika
vikao vya pamoja vya wataalamu vya utafutaji wa ufumbuzi wa matatizo mbali
mbali (Maabara) hapa Zanzibar hapo mwaka jana ikiwa ni pamoja na uhamasishaji
wa utafutaji wa rasilimali, uimarishwaji wa mazingira ya biashara na utalii.
Dk. Shein
alisisitiza kuwa maazimio hayo yamepitishwa katika Bajeti ya mwaka 2014-2015
ambapo utekelezaji wake ulianza Julai mwaka jana ambapo ni miezi sita tu tokea
kuanza utekelezaji huo.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisema kuwa matarajio yaliopo ni kuhakikisha kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mbinu za kuendesha vikao hivyo wa wataalamu (Maabara)
utekelezaji wake unaipeleka Zanzibar kutoka uchumi wa chini na kuelekea uchumi
wa kati.
Dk. Shein
alisema,“Lengo la juhudi hizo ni kuhakikisha Zanzibar inabadilika kuanzia hivi
sasa kutoka katika uchumi wa chini na kuelekea katika uchumi wa kati mnamo
mwaka 2020”.
Alisema kuwa hii
inatoa matumaini kutokana na hivi sasa uchumi wa Zanzibar kuimarika kwa kasi
kwa kiwango cha asilimia 7.4 kwa hesabu za mwaka 2013 ambapo hali inaonesha
kuwa hata mwishoni mwa mwaka 2015 asilimia inaweza kufikia 7.8 ambayo ukuaji wake
ni mkubwa kwa nchi za Afrika Mashariki
sambamba na nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara.
Alisisitiza kuwa
elimu itakayopatikana katika mkutano huo kati ya viongozi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na wataalamu kutoka nchini Malaysia utatoa mwelekeo na mbinu
mpya katika utekelezaji wa matokeo makubwa kwa njia za haraka katika kukuza
uchumi.
Nae Dk. Idris
Jala alieleza mbinu na mikakati iliyowekwa na Malaysia katika kuhakikisha
wanafikia lengo lao la ‘matokeo makubwa kwa njia za haraka’ walizojiwekea katika
kuimarisha uchumi wao sambamba na changamoto zilizojitokeza.
Alisema kuwa
hatua hiyo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa Malaysia huku
akisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya kutosha kati ya sekta ya umma na
sekta binafsi. Aidha alizitaja baadi ya nchi zilizopanua wigo ikiwemo Afrika
Kusini, India, Tanzania, Korea na nyenginezo huku akisisitiza kuwepo mafanikio iwapo
hapatakuwa na urasimu hatua mabayo itatokomeza suala zima la rushwa.
Mapema Mshauri wa
Rais Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alieleza azma ya mkutano huo wa siku
moja pamoja na kutumia fursa ya kutoa wasfu wa wataalamu hao kutoka Malaysia na
Tanzania.
Akifunga kikao
hicho Dk. Shein amewahakikishia wataalamu hao kuwa azma hiyo itafikiwa kwa
mashirikiano ya pamoja na kueleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa dira katika
kufikia malengo yaliowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza
na kuimarisha uchumi wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments