STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Julai, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa mchakato wa kumpata mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho haukutawaliwa na sintofahamu yoyote kama baadhi ya watu wanavyoeneza bali ulizingatia utaratibu na kanuni za uchaguzi za chama hicho.
Akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari katika kiwanja cha Ndege cha Abeid Aman Karume mara baada kuwasili kutoka Dodoma leo, Dk. Shein alisema hakukuwa na mtafaruku wowote na kwamba uteuzi wa wanachama watatu katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama (NEC) hicho waliopigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu ulizingatia sifa za wagombea na mfumo wa demokrasia ya chama ya wengi wape.
“Tulijadili kwa kina sifa za wagombea na kushauriana hadi mwishoni tukafikia makubaliano na ndio maana tulipiga kura kwa utulivu na nidhamu kwa mujibu wa taratibu za chama chetu na kuwapata wana CCM watatu kwenda Mkutano Mkuu” alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa ndio maana majina hayo matatu yalipopelekwa katika Mkutano Mkuu yalipigiwa kura bila ya matatizo yeyote.
Kuhusu kujitokeza kwa wingi wana CCM katika kinyang’anyiro hicho alisema ni kuonesha ukomavu wa demokrasia katika CCM na kufafanua kuwa wagombea nafasi hiyo wamekuwa wakiongezeka tangu chama hicho kilipobuni mfumo huo wa kuwapata wagombea wake mwaka 1995.
Akijibu swali kuhusu nafasi ya wanawake katika chama hicho na madaraka ya umma, Dk. Shein ambaye pia ni Ras wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema CCM na serikali zake inajali fursa za wanawake katika uongozi na haikushangaza uteuzi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM fursa ambayo itamfanya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke nchini.
“Ni uteuzi uliofanywa kuzingatia sifa za mwana CCM huyo (Samia) na dhamira ya nchi yetu ya kutekeleza kwa vitendo sio tu maamuzi ya Jumuiya ya Kimataifa ya kuwa na uwakilishi wa 50 kwa 50 lakini pia azma yetu ya kuwapa nafasi wanayostahiki wanawake katika jamii yetu” Dk. Shein alieleza.
Aliahidi fursa zaidi za kushika madaraka na uongozi kwa wanawake katika Serikali za awamu zijazo mara baada ya Chama cha Mapinduzui kushinda uchaguzi mwezi Oktoba mwaka huu.
Katika mnasaba huo alimpongeza Mgombea Urais wa CCM katika kinyang’ayiro cha nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano Dk. John Pombe Magufuli kwa kumpendekeza Mheshimiwa Samia kuwa mgombea Mwenza wake na kumwagia sifa Dk. Magufuli kwa uhodari na umakini wake katika kutumikia taifa.
Kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya wananchi wananyimwa vitambulisho vya ukaazi na hatimae kukosa kupiga kura, Dk. Shein alieleza kushangazwa na baadhi ya wanasiasa kuwapotosha wananchi hao kwa kutaka suala hilo lishughulikiwe kisiasa badala ya kufuata sheria zilizopo ambazo zimeweka wazi utaratibu mzima wa suala hilo.
“Baadhi ya wanasiasa wanajisahau na kuwapotosha wananchi. Sheria haikusema wanasiasa washughulikie matatizo ya vitambulisho badala yake imeelekeza wananchi wenyewe wafanye hivyo kwa mujibu wa sheria zilizopo na wako huru hata kutumia wakili kudai haki yao” Dk. Shein alisisitiza.
Dk. Shein alisema si sahihi hata kidogo kwa baadhi ya wanasiasa kutaka kuonesha kama kwamba Rais ndie anayetoa vitambulisho hivyo matokeo yake kumbebesha lawama zisizo na msingi.
Aliwasihi wananchi walio na malalamiko kuwa wanapaswa kulalamika wao wenyewe kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo na kuwahakikishia kuwa hakuna atayenyimwa haki yake kama anastahiki.
Hata hivyo alisema ni kweli usiopingika kuwa baadhi ya wananchi wanalazimisha kupatiwa vitambulisho hivyo hali ya kuwa si wakaazi wa maeneo husika kwa kuwa sheria inamtaka mhusika ili kupatiwa kitambulisho awe mkaazi wa eneo husika kwa angalau miezi 36.
Katika mahojiano hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwasihi waandishi wa habari kuzingatia uzito wa kazi yao katika kipindi hiki ili kuelimisha wananchi kwa usahihi bila ya kuwa sehemu ya kupotosha jamii.
“waandishi mnapaswa kuwa na subira na kuonesha umakini wenu kwa kila mnachokitangaza na kukiandika ili wananchi waelimike na hatimae waweze kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi ujao” Dk. alisema.
Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pamoja na kupendekeza majina matatu ya wana CCM waliowania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipitisha pia jina la Dk. Shein kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
0 Comments