STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 14.10.2015
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Ali Mohammed
Shein ameeleza azma yake ya kuendelea kuwainua wasanii hapa nchini kwa
kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa studio za kisasa ambazo tayari zimekamilika
na kuwekwa vifaa vyenye sifa na ubora wa pekee kwa shughuli za kurikodia.
Dk. Shein aliwataka wasanii hao kukaa mkao
wa kula kwani lengo lake la kuwainua wasanii limefikiwa ambapo tayari ujenzi wa
studio hizo za kisasa za kurikodi nyimbo na michezo ya kuigiza umekamilika na wakati
wowote shughuli za kurikodi zitaanza.
Hayo aliyasema wakati alipokuwa
akizungumza na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano wa
Kampeni za uchaguzi kwa upande wa CCM uliofanyika katika uwanja wa mpira Chwaka,
Jimbo la Chwaka, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema
kuwa studio hizo zimejengwa kwenye jengo jipya la zamani la Utangazaji la Sauti
ya Tanzania Zanzibar, baada ya kufayiwa matengenezo makubwa na kuwekewa vifaa hivyo vya kisasa.
Alisema kuwa lengo na madhumuni ya ujenzi
wa studio hizo ni kuhakikisha wasanii wanaimarisha kazi zao za sanaa zao na
kwenda na wakati uliopo kutokana na vifaa vya kisasa vilivyomo ndani ya studio
hizo.
Dk. Shein alisisitiza kuwa wasanii
watafaidika na huduma zitakazotolewa na studio hizo ambazo zitawasaidia
kuondokana na usumbufu wanaoupata hivi sasa katika kurikodi kazi zao.
Studio hizo ni za kisasa ambazo ni za
pekee kwa nchi za Afrika Mashariki ambapo vifaa vyake vinatoka nchini Uingereza
na tayari vifaa hivyo vimeshafanyiwa majaribio na wakati wowote shughuli za
kurikodi kazi za wasanii zinatarajiwa kuanza.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments