Wazazi na walezi wa kijiji cha Mto wa pwani wametakiwa kushirikiana na Walimu na kamati ya skuli ili kuhakikisha watoto wao wanapata maendeleo mazuri katika masomo yao.
Hayo yameelezwa na Mwalimu wa Skuli ya Mto wa Pwani Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja Jabu Said Abass wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika Skuli hiyo.
Amesema kuwa suala la kuwasimamia wanafunzi katika masomo siyo la walimu pekeyao bali Wazazi wanajukumu la kuwasaidia Watoto wanapokuwa nyumbani.
Ameeleza kuwa Watoto wengi wanafeli kutokana na Wazazi kutofuatilia maendeleo ya Watoto wao hivyo ipo haja kwa Wazazi kujenga tabia ya kuwasaidia watoto badala ya kuwaachia kutumia muda mrefu kuangalia michezo katika Televisheni.
Mmoja ya wazee wa skuli hiyo Amina Jecha Bakari amekiri kuwa mashirikiano baina ya wazazi na walimu wa skuli hiyo ni madogo na amewaomba wazazi wenziwe kuwa karibu na walimu katika kuwapatia watoto haki yao ya elimu kwani ndiyo nguvu kazi ya Taifa la baadae.
Sheha wa Shehia ya Mto wa pwani Omar Ali ameiomba Serikali kuwajengea madarasa mengine ili wanafuzi wasiende masafa ya mbali kufuata skuli.
Amesema katika skuli hiyo kuna madarasa sita yanayotumiwa na wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa la nne na wanapoingia darasa la tano hulazimika kwenda skuli ya Pale kutokana na upungufu wa madarasa.
0 Comments