6/recent/ticker-posts

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Abeida Rashid Apongeza Jitihada za Dawati la Jinsia na Watoto

 


Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Abeida Rashid Abdallah, amepongeza utendaji kazi wa maafisa wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi, kwa kujitoa kwao katika kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya kikao kazi cha pamoja kati ya watendaji wa Dawati hilo na Wizara, yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi Zanzibar, Katibu Mkuu huyo alisema “Mafunzo haya ni muhimu sana kwani yametoa dira ya kuendeleza mashirikiano imara kati ya Jeshi la Polisi na Wizara inayosimamia ustawi wa jamii nzima ya Zanzibar.”

Aidha, amewataka maafisa hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii, hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii, ambavyo vinaendelea kuathiri maisha ya watu, hususani vijana, watoto,  wanawake na wazee.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jonas M. Mahanga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, amesisitiza kwamba “Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto wataendelea kutoa huduma bora kwa jamii na kuboresha zaidi huduma hizo kwa kutumia mbinu za kitaalamu walizopata kupitia mafunzo mbalimbali.

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi Faidha Suleiman, Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Makao Makuu Dodoma, alieleza kuwa, Jeshi la Polisi limeweka watendaji wa dawati hilo katika vituo vyote vya Polisi nchi nzima, ambapo hadi sasa kuna jumla ya madawati 420 Kati ya hayo  Zanzibar, ina madawati 42, na maandalizi yanaendelea kufanyika ili kupanua huduma hizo hadi viwanja vya ndege na Bandari zote za Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Stafu Sajini wa Polisi Khamis Khamis, amewashukuru wadau wote wakiwemo SOS Children’s Village kwa kuwezesha mafunzo hayo muhimu ambayo yamewajengea uwezo wa kuwa walimu bora wa kutoa elimu kwa jamii na kusaidia kutokomeza vitendo vya  udhalilishaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Imetolewa na:

Kitengo cha Habari

Makao Makuu ya Polisi –Kamisheni ya Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments