6/recent/ticker-posts

Serikali Inaendelea Kufanya Mageuzi Katika Sekta Mbalimbali Kwa Lengo la Kuleta Maendeleo Nchini


Na Imani Mtumwa   Maelezo    29.12.2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi
 na Utawala Bora, Dkt.Mwl. Haroun Ali Suleiman, amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo nchini, hususan katika sekta ya makazi.

Ameyasema hayo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu Kwa Mchina Mwazo Awamu ya Pili, Wilaya ya Magharibi B, ikiwa ni muendelezo mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dkt. Haroun amesema mageuzi hayo yalianza tangu awamu ya kwanza ya uongozi na yaliendelea katika awamu zilizofuata, huku Serikali ya Awamu ya Nane ikiimarisha zaidi miundombinu yote kwa lengo la kuwapatia wananchi makazi bora na yenye hadhi.

Amesema mradi huo pia umesaidia kutoa ajira kwa vijana, hatua inayowawezesha kujipatia kipato sambamba na  kuwataka kuzitunza vizuri nyumba hizo ili zidumu kwa muda mrefu.

Aidha, Dkt. Haroun amewasihi vijana kuendelea kudumisha uzalendo kwa kulinda amani ya nchi, ili Serikali iweze kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar Ndg Sultan Said Suleiman, amesema Mradi wa Nyumba za Kisasa za Mombasa kwa Mchina – Awamu ya Pili una lengo la kuongeza upatikanaji wa makazi bora, salama na yenye hadhi kwa wananchi Samabamba, na kuimarisha mazingira rafiki kwa shughuli za biashara na huduma za kijamii.

Amefafanua kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa jumla ya nyumba 22 za kisasa, zitakazojumuisha maeneo ya biashara katika ghorofa ya chini, maeneo ya maegesho ya magari pamoja na eneo la bustani kwa watoto.

Ameongeza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliyesisitiza matumizi bora ya ardhi kwa kujenga majengo ya ghorofa badala ya kuendelea na ujenzi holela usiozingatia mipango ya miji.

Ndg Sultan amesema utekelezaji wa mradi huo unafanywa na Kampuni ya Emirates Contractor, chini ya usimamizi wa karibu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar kama mshauri mkuu, ili kuhakikisha kazi zote zinafanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora, usanifu uliopangwa na masharti ya mkataba.

Awali alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa uongozi wake thabiti, maono makubwa na jitihada zake katika kuimarisha sekta ya makazi kupitia Shirika la Nyumba la Zanzibar.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 3.8, zikihusisha kazi za ujenzi, miundombinu ya huduma muhimu ikiwemo umeme na maji, pamoja na maandalizi ya mazingira ya mradi.





Post a Comment

0 Comments