Mkurugenzi Mtendaji wa Equity For Tanzania Limited- EFTA Bwana Nicomed Bohay akizungumza na wageni waalikwa wakati wa uzindunzi wa Hati Fungani za EFTA tukio lilofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam katika Hotel ya Kilimanjaro Hyatt Regency. 







.jpeg)
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA) imezindua
rasmi Hati Fungani ya Shilingi bilioni 50, hatua inayotajwa kuwa kichocheo cha
kuunganisha masoko ya mitaji na sekta halisi za uzalishaji kama kilimo,
usafirishaji na viwanda.
Uzinduzi huo umeofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam, uliwakutanisha wadau wa sekta ya fedha, wawekezaji na
taasisi mbalimbali za kifedha, huku ujumbe mkuu ukiwa ni kuimarisha upatikanaji
wa mtaji wa muda mrefu kwa shughuli zinazozalisha mapato.
Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, alisema Hati
Fungani hiyo imelenga kuhakikisha kampuni inapata mtaji wa muda mrefu
unaoendana na maisha ya mali zinazofadhiliwa.
“Tunafadhili mali kama matrekta, magari ya biashara na
mitambo ya viwandani ambayo huzalisha mapato kwa miaka kadhaa. Kupitia Hati
Fungani hii tunahakikisha tunapata mtaji wa muda mrefu unaoendana na maisha ya
mali hizo,” alisema Bohay.
Kwa mujibu wa Bohay, fedha zitakazokusanywa zitaelekezwa
moja kwa moja katika kupanua huduma za ukodishaji wa mali (leasing) kwa
wakulima, wasafirishaji, wakandarasi pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa
kati. Lengo ni kuongeza uwezo wa uzalishaji kwa kuwapatia zana na mitambo
inayowawezesha kufanya kazi kwa tija zaidi.
Mchumi wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA), Profesa Andrew Temu, alisema upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu ni
nyenzo muhimu katika kuchochea mapinduzi ya uzalishaji barani Afrika.
“Afrika haina tatizo la uhitaji wa vifaa vya uzalishaji;
changamoto ni namna ya kuvipata. Taasisi kama hizi zikipewa mtaji wa muda
mrefu, zinaweza kusaidia wakulima na wajasiriamali kupata mitambo kwa urahisi
zaidi,” alisema Prof. Temu.
Aliongeza kuwa mitaji ya muda mfupi mara nyingi haiendani na
mahitaji ya uwekezaji katika sekta za uzalishaji, hasa kilimo na viwanda,
ambavyo vinahitaji muda mrefu ili kurejesha faida. Hivyo, uwepo wa Hati Fungani
kama hii unasaidia kuleta uwiano kati ya muda wa uwekezaji na muda wa
marejesho.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana (CMSA) David Magabe alisema utoaji wa Hati Fungani unaongeza kina
cha soko la mitaji na kusaidia kuelekeza akiba za ndani kwenye shughuli za
uzalishaji, badala ya kubaki katika mifumo ya uwekezaji isiyogusa moja kwa moja
uchumi halisi.
Hati Fungani hiyo inatoa riba ya ushindani ya asilimia 14
kwa mwaka na uwekezaji unaanzia Shilingi 500,000, hatua inayolenga kupanua
ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji unaochochea sekta za uzalishaji.
Kwa kuunganisha mitaji ya wawekezaji na mahitaji ya
wakulima, wasafirishaji na wamiliki wa viwanda, uzinduzi wa Hati Fungani ya
EFTA unaashiria hatua mpya ya kutumia masoko ya mitaji kama daraja la
kuimarisha uchumi halisi wa Tanzania.
Mwisho




0 Comments