Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake watahakikisha wanalipa kipaumbele suala la tahfidh qur-ani ndani ya Jimbo la Kiwani.
Ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa madrasat Thamarat Jamii na madrasatu Thamarat Jannah zilizomo katika Shehia ya Mwambe Jimbo la Kiwani Pemba.
Amesema katika kuhakikisha elimu ya Qur-an inaimarika zaidi jimboni humo uongozi wa Jimbo wamejipanga kuweka mazingira bora, salama na rafiki kwa walimu na wanafunzi kuweza kukisoma na kukihifadhi kitabu cha Qur-an ambacho kinatoa muongozo na mafundisho katika maisha ya dunia na akhera.
Mhe. Hemed amesema ndani ya jimbo la kiwani kuna jumla ya madrasa 90 ambapo viongozi wa Jimbo wamejipanga kuzijenga upya na kuzifanyia ukarabati madrasa ambazo mazingira yake sio rafiki kwa wanafunzi kuendelea kujisomea jambo ambalo litatoa fursa kea walimu na wanafunzi kukiendeleza kitabu kitukufu cha Qur-an kwa midingi inayotakiwa.
Aidha, Mwakilishi huyo wa Jimbo la Kiwani amewataka wazazi na walezi kuwalea vijana wao katika maadili mema na kuwahimiza kufanya mambo ya kheri ikiwemo kukisoma na kukihifadhi kitabu kitakatifu cha Qur-an na mafundisho ya bwana Mtume Muhammad (S.A.W ).
Sambamba na hayo, Mhe. Hemed amewahimiza wananchi wa Jimbo la Kiwani kuendeleza umoja, upendo na mshikamano na kuwa tayari kutoa mashirikiano kwa viongozi wa Jimbo ili kufanikisha azma ya maendeleo kwa wote jimboni humo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya walimiu na wanafunzi wa madrasa hizo, Mzee Juma Adibu amemshukuru Mhe. Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani na kuwaombea dua viongozi wakuu ili waweze kupata nguvu ya kutatekeleza yale yote waliyoyaahidi kwa wananchi.
Mzee Adibu amewataka wanachi wenzake kuendeleza mshikamano walionao na kuendelea kuwaunga mkono viongozi katika harakati mbali mbali za maendeleo.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiambatana na viongozi wenzake wametembelea bonde la Mpunga la KWA JOMBWE KWA SHAVUAI kukagua namna wananchi wanavyopatiwa huduma ya kulimiwa mashamba yao kwa Trekata la Jimbo la kiwani ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyowaahidi wakulima jimboni humo kwamba watakapomchagua kuwa mwakilishi wao atawapatia Trekta ambalo litawalimia bila ya malipo yoyote.
Mhe. Hemed amesema jumla ya hekta 123.25 zimeshalimwa na wananchi 295 wameshapatiwa huduma ya kulimiwa mashamba yao ambapo matarajio makubwa ni kuhakikisha sekta ya kilimo inaimarika zaidi jimboni humo.
Amewataka maafisa wa kilimo kiwapatia elimu wananchi juu ya kulima kilimo cha kisasa chenye tija kitakacho wanufaisha zaidi wakulima lakini pia kusogeza huduma za pembejeo karibu na mashamba ya wakulima ili kuwapunguzia changamoto ya kufuata pembejeo hizo masafa ya mbali.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Pemba Muhandisi Idriss Hassan Abdalla ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaloyotolewa na Mhe. Makamu wa Pili wa Rais ikiwemo kuwapatia elimu wakulima, kusogeza karibu huduma za pembejeo na kushirikiana na wakulima katika kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika sekta ya kilimo jimboni humo .
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe …07 / 02 / 2026
0 Comments