Wazazi na walezi wametakiwa kushirikiana na walimu wa madrasa katika kuwalea vijana kwa kufuata misingi ya dini ya kiislamu na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad (S.A.W ) ili kupata kizazi chema.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla katika maadhimisho ya Maulid ya kuzaliwa kwa mtume Muhammad (S.A.WA ) yaliyoyanyika katika Mtaa wa BAKWATA Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.
Amesema kuwalea vijana katika malezi bora yenye kufuata mafundisho yaliyomo ndani ya kitabu kitakatifu cha Qur-an pamoja na kuwapatia elimu yenye manufaa kutapelekea kupata kizazi chema chenye kumcha Mwenyezimungu na kumtukuzaa mtume Muhammad ( S.A.W ).
Alhajj Hemed amefahamisha kuwa ni lazima wazazi kushirikiana na walimu wa madrasa katika kuhakikisha wanaendeleza kusoma maulid kila mwaka ili kuendelea kudumisha mila na silka za kiislam kama walivyofanya wanazuoni waliotangulia.
Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza waumini wa dini ya kiislam na wananchi wa Tanga kwa ujumla kuendelea kuliombea dua Taifa pamoja na viongozi wakuu wanchi ili kuweza kupiga hatua kimaendeleo kwa maslahi mapana ya vizazi vya sasa na baadae.
Aidha makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisistiza wananchi wa Wilaya Pangani na wanatanga kwa ujumla kuendelea kusimama katika maendeleo na kutokubali kurubuniwa na watu wachache wasiopenda maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Pangani ambae pia ni Waziri wa Maji wa Tanzania Mhe. JUMAA HAMID AWESU ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maendeleo makubwa yanayopatikana kwa wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Amesema kuwa serikali imejenga miradinmbali ya maendeleo ikiwemo barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tanga mjini hadi Pangani, maji safi na salama sambamba na kuwapatia vitendea kazi wavuvi wa maeneo hayo ili kuweza kufanya shuhuli zao za kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.
Aidha Mhe. Awesu ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka boti ya mwendo kasi baina ya Zanzibar na Tanga kupitia bandari ya Pangani ili kuweza kuifungua Pangani kiuchumi na kupata maendeleo zaidi.
Nae Sheikh Rajab Abrahman Abdalla amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuwajali na kuwathamini wananchi wa Mkoa wa Tanga na kuendelea kuwapa ushirikiano mkubwa hasa katika shughuli za kimaendeleo.
Amesema kuwa wananchi wa Pangani wanaishi kwa umoja, upendo na mshikamano na kuahidi kuwa wataendelea kufanya hivyo ili vizazi vijavyo viweze kurithi tunu hio ya umoja na mshikamano uliopo kwa wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj. Hemed Suleiman Abdulla aakizungumza na viongozi mbali mbali, Masheikh, waumini wa dini ya kiislam na wananchi wa Wilaya ya Pangani katika maadhimisho ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W ) yaliyofanyika Jana tarehe 04.02.2026 katika Mtaa wa Bakwata, Pangani Mkoani Tanga.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe..05.02.2026.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
0 Comments