6/recent/ticker-posts

Taasisi ya Elimu Zanzibar kuimarisha elimu kwa watoto wenye ulemavu wa akili



MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) Abdalla Mohamed Mussa amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha elimu kwa watoto wenye ulemavu wa akili kwa kuandaa na kuanza kutekeleza mtaala rekebifu unaolenga kuwagusa moja kwa moja kulingana na mahitaji yao ya kujifunza.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya uchambuzi wa mtaala rekebifu na vifaa vyake yanayofanyika Skuli ya Msingi Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa waalimu wanaoshughulika na watoto wenye mahutaji maalumu wa mkoa huo.
Alisema jitihada hizo ni matokeo ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa wazazi ambao watoto wao hapo awali walikuwa wakisoma katika mfumo wa elimu jumuishi lakini wakionekana kutofanya vizuri kitaaluma kutokana na kutokuwepo kwa mtaala unaozingatia hali zao.
Alieleza kuwa wataalamu wameigawa akili katika makundi makuu manne yanayotofautiana, hali iliyosababisha kuandaliwa kwa mtaala maalumu ili kila kundi liweze kuhudumiwa ipasavyo na kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Aidha, alieleza kuwa kuwawekea watoto wenye ulemavu wa akili mtaala wao maalumu haina maana ya kuwabagua, bali ni njia ya kuwazingatia mahitaji yao ili waweze kufanikiwa kielimu kama wengine.
Alisisitiza kuwa huu si mwanzo wa utekelezaji wa mtaala huo, bali ni sehemu ya mchakato unaoendelea, ambapo changamoto hugunduliwa wakati wa utekelezaji na kutafutiwa ufumbuzi kupitia majadiliano, mashauriano na ushirikiano wa wadau wote wa elimu, ili kufikia mafanikio.
Sambamba na hayo alisema kuwa walimu ndio wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa mtaala huo, hivyo wanapaswa kuzitilia mkazo jitihada za Serikali ili zisiwe za bure, kwa kuutekeleza kikamilifu na kwa kushirikiana na wazazi katika kuwafichua na kuwahamasisha watoto wenye ulemavu kuhudhuria skuli.
Mapema.Ofisa Mkuza Mitaala wa TEZ, Ali Mjaka Haji, alisema mafunzo hayo ya siku sita yamelenga kuwajengea uwezo walimu wanaoshughulika na watoto wenye ulemavu wa akili kutoka Mkoa wa Kaskazini ili waweze kusimamia na kutekeleza mtaala huo kwa ufanisi.
Alisema baada ya mafunzo hayo, waalimu watapata uelewa wa kina juu ya namna ya kujitathmini, kutambua makundi ya wanafunzi waliyonayo na kuchagua mbinu sahihi za ufundishaji kulingana na hali za wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Skuli ya Msingi Mahonda, Salha Abdulla Salum, alisema mtaala huo utawasaidia wanafunzi kupata mahitaji yao yote ya kujifunza kulingana na hali zao, jambo litakaloongeza hamasa kwa watoto waliokuwa wakibaki majumbani pamoja na kuwajengea wazazi imani juu ya maendeleo ya watoto wao.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa iliyokuwepo awali ni ukosefu wa vifaa na miongozo ya kufundishia watoto wenye ulemavu wa akili, hivyo mtaala huo unatarajiwa kuwa mwarobaini wa changamoto hizo na kuhakikisha haki na usawa kwa wanafunzi wote
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano (TEZ).



 

Post a Comment

0 Comments