6/recent/ticker-posts

Wanachama ACT Wazalendo Wapo tayari kupokea maamuzi





Wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo wamesema wako tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayofikiwa na viongozi wao katika juhudi za kutafuta muafaka wa kudumu wa kisiasa Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa katika kikao maalumu cha kuwaeleza wanachama maendeleo ya mazungumzo kati ya ACT-Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa chama hicho kisiwani Pemba, Mratibu Rashid Ali Abdallah alimhakikishia Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, kuwa wanachama wana imani kamili na uongozi wao.
“Ndugu Mwenyekiti, sisi wanachama wako hatuna shaka na wewe pamoja na viongozi wenzako. Tuko tayari kupokea maamuzi yoyote mtakayotuletea,” alisema Rashid.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkoa wa Wete kichama, Juma Khamis Ali maarufu Kabakaba, alisema yeye pamoja na wanachama wa mkoa huo hawana shaka na maamuzi yatakayofanywa na viongozi wa kitaifa.
“Tunaelewa viongozi wetu ni wazalendo wanaopenda maslahi ya Zanzibar na wananchi wake. Hatuoni sababu ya kuwa na shaka kwa watakayotuletea,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti Chama hicho Zanzibar Ismail Jussa alisema imani wanaoionyesha wafuasi wa chama hicho kwa viongozi ndio inayopelekea chama hicho kunawirika kila uchao
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, alisisitiza umuhimu wa Wazanzibari kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti za vyama vya siasa.
Alisema migogoro ya kisiasa huwapa nafasi maadui kuingiza maslahi yao, hivyo umoja ni muhimu kwa ustawi wa taifa.
“Lazima Wazanzibari tuwe kitu kimoja na tulinde nchi yetu ili adui asipate nafasi,” alisema Othman.
Alieleza kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) itakayojenga mshikamano na kupigania maslahi ya wananchi.
Aidha, aliishukuru timu ya mazungumzo ya chama hicho, huku akitoa shukrani maalumu kwa Mwenyekiti mstaafu, Juma Duni Haji, kwa mchango wake mkubwa katika mchakato wa kutafuta muafaka wa kudumu Zanzibar.
Othman alisema pande zote zimekubaliana kurejea katika vyama vyao kukamilisha taratibu za ndani kabla ya kutoa taarifa ya pamoja, huku wakiahidi kurejesha imani ya wananchi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.
Miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa ni pamoja ni kutungwa kwa Katiba Mpya Kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa na mamlaka kubaki mikononi mwa wananchi
Kuimarisha mfumo wa uwajibikaji kwa viongozi
Kufanyia mapitio mfumo wa uchaguzi ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima
Aliongeza kuwa kutakuwa na utaratibu maalumu wa utekelezaji wa makubaliano hayo mara baada ya taratibu za ndani za pande zote kukamilika.
“Tunataka Serikali ya Umoja wa Kitaifa iwe ya pamoja kweli kweli, ili kila mmoja afurahie matunda yake,” alisema.
Aliwaomba wanachama kuwa na subira wakati taratibu zikikamilishwa, ndipo uamuzi wa kuingia au kutokuingia serikalini utafanyika rasmi.
“Kama mlivyoahidi kuwa hamna hofu na viongozi wenu, basi tuendelee kuwa pamoja ili tufanye mambo yetu kwa usalama,” alihitimisha Othman Masoud Othman.
Imetolewa na Idara ya Habari na Uenezi.ACT Wazalendo.


 

Post a Comment

0 Comments