6/recent/ticker-posts

CCM Imejipanga Kudhibiti Baadhi ya Wanachama Kudhibiti Maadhi Wanachama Wanaojaribu Kuanzisha Makundi Yasiyofaa -Dkt.Dimwa

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza katika hafla ya futari ya Madiwani wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja iliyofanyika katika ukumbi Kibweni, Zanzibar.

NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema chama hicho kimejipanga kudhibiti baadhi ya wanachama wanaojaribu kuanzisha makundi yasiyofaa yanayoweza kuchochea migogoro kuelekea uchaguzi mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Dkt. Dimwa, alieleza kuwa tayari kuna dalili za baadhi ya wanachama kuanza vuguvugu la kujipanga katika makundi yenye lengo la kuwachafua wenzao kupitia mitandao ya kijamii na vikao visivyo halali, ikiwa ni mkakati wa kuwawezesha watu wao wachache kupata uongozi ndani ya chama kinyume na utaratibu.

Alisisitiza kuwa vitendo hivyo vinakwenda kinyume na katiba, kanuni na miongozo ya CCM ambayo inaweka utaratibu wa kufanya maamuzi kupitia vikao halali na mamlaka husika.

Akizungumza katika futari ya madiwani wa Mkoa wa Mjini Magharibi iliyofanyika Kibweni, Dkt. Dimwa alisema kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi, lakini ni lazima afuate taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha haki ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa inalindwa.

Alionya kuwa chama kimeanza kufuatilia kwa karibu mienendo ya wanachama wanaojihusisha na vitendo vya kuchafuana, na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka maadili ya chama, ikiwa ni pamoja na wale wanaojihusisha na udalali wa kisiasa unaohatarisha hadhi ya CCM.

“Ndani ya CCM hatutavumilia vitendo vya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi, wanaotumia nafasi zao kuchafua wenzao au kusaka maslahi binafsi kwa gharama ya chama,” alisisitiza Dkt. Dimwa.

Aidha, alifafanua kuwa uwepo wa makundi wakati wa uchaguzi ni jambo la kawaida kisiasa, lakini kwa utamaduni wa CCM, makundi hayo yanapaswa kufa mara baada ya uchaguzi kumalizika na wanachama wote kurejea kuwa kitu kimoja chenye lengo la kulinda maslahi ya chama.

Aliongeza kuwa dhamira yake ni kuona CCM inapata viongozi waadilifu, wachapakazi na wazalendo, badala ya viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuvuruga misingi ya chama.

Katika hatua nyingine, Dkt. Dimwa alimpongeza Mstahiki Meya wa Baraza la Mji wa Zanzibar, Mohamed Ibrahim Hassanali 'Raza Lee', kwa kuandaa futari hiyo iliyowakutanisha viongozi na wananchi, akibainisha kuwa Ramadhani ni kipindi muhimu cha ibada na kutenda mema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Ali Abdalla, aliwasihi madiwani kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Mstahiki Meya, Mohamed Ibrahim Hassanali “Raza Lee”, alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa madiwani, akieleza kuwa futari hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano na kubadilishana mawazo yenye tija kwa maendeleo ya jamii.

CAPTION

Picha no.88- NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza katika hafla ya futari ya Madiwani wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar iliyofanyika Kuibweni, Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments