Mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana katika sekta ya Afya yanatokana na udhibiti bora wa magonjwa ya kuwambukiza, upanuzi wa programu za chanjo na maboresho makubwa katika huduma za mama na mtoto.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Mkutano wa SPARK –NCD na Ushirikishaji taarifa za tafiti za huduma Jumuishi za UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza kwa nchi za Afrika unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Ameeema licha ya mafanikio hayo, Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa ya magonjwa sugu duniani yakiwemo sindikizo la damu na kisukari ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatuwa za haraka na za kimkakati ili kupambana na magonjwa hayo.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa programu ya SPARK-NCD inalenga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, majeraha, afya ya akili, kujenga wafanyakazi wenye ujuzi wa Afya ya Umma, kuingiza ufuatiliaji wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndani ya mifumo ambayo itasaidia nchi katika kuasisi huduma jumuishi kwa kiwango kikubwa.
Aidha, amezishauri nchi wanachama na washirika wote kuipa kipaombele mifumo jumuishi ya ufuatiliaji wa data na kuongeza nguvu kazi itakayohakikisha ushirikiano na taasisi za ufuatiliaji unakuwa endelevu kwa ukuwaji wa sekta ya afya na wananchi kwa ujumla.
Hata hivyo, amewasihi washiriki wa Mkutano huo kuangalia vipaombele muhimu vya sera na ufadhili pamoja na kuweka mikakati ya kuzidisha ushirikiano wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na fursa za kuchunguza mifumo endelevu ya ufadhili.
Nae Dkt. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu ambae pia ni Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa kiafya kupitia ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, imeimarisha miundombinu ya Hospitali nchini, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Afya na kuunganisha upimaji wa VVU katika huduma za msingi.
Dkt. Mkuya amefahamisha kuwa Programu ya SPARK inalenga katika uimarishaji wa Kinga na hatua dhidi ya vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuzingatia uhamasishaji wa jamii, ushirikiano wa sera na kuchochea mabadiliko katika bara zima la Afrika.
Amesisitiza kuwa Ushirikiano wa wafadhili na wadau mbali mbali wa Sekta ya Afya utawezesha kujenga mifumo thabiti ya afya inayozuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuhakikisha familia zenye afya, uchumi imara na mustakabali mwema wa Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji Wizara ya Afya Zanzibar dkt. Amour Suleiman Mohammed amesema Mikutano huo utajadili mambo mbalimbali ikiwemo namna bora ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuyapatia suluhisho la kudumu.
Dkt. Amour amesema ili kupambana na magonjwa hayo kunahitajika kuwepo kwa mfumo wa ufuatiliaji na data ambao utahifadhi takwimu muhimu zitakazotumika katika katika kukabiliana na magonjwa hayo.
Amefahamisha kuwa katika mapambano hayo nguvu kazi ya wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo yakuambikiza inahitajika katika kufikisha huduma za kiuchunguzi na kitabubu kwa watu wanasumbuliwa na magonjwa hayo jambo litakalochangia kupungua kwa kasi ya magonjwa hayo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika Dkt.M0hammed Abdul-Azizi amesema mkusanyiko huo uliowakutanisha viongozi, watunga Sera na wataalamu mbalimbali kwa lengo la kujadili namna ya kujikinga na kupata suluhisho la muda mrefu la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yamekuwa ni kikwazo kikubwa kwa Bara la Afrika.
Amesema kadiri magonjwa hayo yanavyozidi kuongezeka Barani Afrika yanatoa mwako kwa SPARK- NCD kuweka mikakati Imara na kuwekeza katika Afya ya jamii sambamba na kuchukua hatua madhubuti za kupambana na magonjwa hayo ikiwemo kutoa elimu kwa jamii na kuwapatia ujuzi watendaji wa Afya juu ya kutowa huduma bora kwa walengwa.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 27 / 03 / 2026
0 Comments