Vijana wetu leo wameonesha ushujaa kama lilivyo jina lao baada ya kuwabwaga Chipolopolo ya Zambia kwa mikwaju ya tuta.
Mchezo ulimalizika katika dakika 90 matokeo yakiwa bado ni bila kwa bila. Muda wa nyongeza pia haukuzaa goli kwa kila timu na Hatimaye mikwaju ya Penelti ilibidi iamue mchezo.
Siku ya leo shujaa alikuwa Magolikipa Mwadini na golikipa wa akiba Mohammed Khamis Juma ambae aliweza kuipangua penelti ya mwisho ya wanachipolopolo na hivyo kuipeleka Heroes nusu fainali. Matokeo yalikuwa Penelti 4-3. Mwadini alicheza dakika tisini za mchezo na Mtaalamu wa kuzuia mikwaju ya penelti Mohamed Juma aliingia badala yake.
Waliofunga penelti zao ni Othman Khamis, Nassor Jamim , Abdul halim Humoud na Aggrey Morris. Alyekosa na Hassan Salum. Waliokosa kwa upande wa Zambia ni Charles Siyengwa na Denis Banda.
Kocha mzalendo Hemed Morocco aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza na timu ngumu kama ya Zambia na kuweza kuwadhibiti kwa muda wote wa mchezo. Ikumbukwe Zambia ilishinda michezo yake yote mitatu iliyocheza na ndiyo timu iliyokuwa ikiogopewa hasa kwa kuweza kuwa ni miongoni mwa timu zilizofuzu Fainali za Africa CAN huko Angola Januari mwakani. Na kuwa ni miongoni mwa timu zilizopewa nafasi kubwa ya kufika fainali.
Kocha Morocco alizidi kuhakikisha kwamba wembe uliomnyoa Zambia ndio utakaotumika kwa kikosi chochote atakachokabiliana nacho na hatoogopwa mtu kwa sababu ya jina la nchi.
Na Kapteni Abdi Kassim "Babi" nae amesisitiza kwamba wamashatimiza ahadi na tayari wameshavuka lengo lao kilichobakia sasa ni kuhakikisha timu watakayocheza nayo ijue inacheza na timu gani.
Zanzibar Heroes itavaana na Uganda katika mchezo wa nusu fainali ambao waliweza kuwaondoa Kenya Harambee Stars kwa goli moja kwa bila.
Kinachonishangaza ni timu hii ambayo ilikuwa na hatihati ya kushiriki kutokana na ukosefu wa fedha. Ni timu hii ambayo haikupata maandalizi ya maana hata kupata mechi ya kujipima nguvu. Sasa iko nusu fainali.
Nadhani Fifa sasa waanze kufikiri tena ombi letu la kuwa mwanachama maana kama hawataki kutusikiliza mezani basi tunaweza kuwaonesha kivitendo kwamba soka letu sasa si la kubahatisha.
Pia Kocha wa Taifa Stars sijui anajifunza nini hapa kwamba huku Zanzibar vipaji vipo si kujaribu kuwapa nafasi wachache katika wachezaji wetu.
Kila la heri Zanzibar Heroes
No comments:
Post a Comment