Na Ismail Mwinyi
MWAKILISHI wa Jimbo la Fuoni Thuwaiba Edington Kisasi, juzi amekizindua kikundi cha mazoezi cha Mandela huku akihimiza wananchi kutodharau kufanya mazoezi kwa faida yao kiafya.
Kisasi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, amewaambia wanachama wa kikundi cha Mandela chenye maskani yake Pangawe Wilaya ya Magharibi, kuwa mazoezi ni njia muafaka ya kuimarisha mwili na kuuweka mbali na maradhi mengi.
“Mwili unaofanya mazoezi, ni tafauti na ule usiojishughulisha, afya njema hupatikana kutokana na mazoezi, hivyo ni vyema kila mmoja akajua umuhimu wa kushiriki”, alisisitiza.
Aidha aliwashauri wanamichezo kujenga ushirikiano kwa ajili ya kuviimarisha vikundi vyao pamoja na kushikamana katika mambo mbali mbali ya kimichezo.
Naye Naibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis, aliwaahidi wanamichezo hao kuwa Wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha kwao katika jitihada za kukuza michezo hapa nchini.
Katika risala ya wanachama wa kikundi hicho iliyosomwa na Naibu Katibu wake Kassim Juma Othman, walisema ni vyema jamii ikaungana katika vikundi vya mazoezi kwani mbali na kuenga mwili, vinasidia kuwaondoshea mataizio ya kijamii kwa kutmia ushirikiano wao.
Hata hivyo, waliiomba serikali kuzingatia umuhimu wa kutenga viwanja vya kufanyia mazoezi ili kiviondoshea usumbufu vikundi vinavyoendelea kuanzishwa hapa nchini.
Mandela Group, kimeanzishwa mwaka 2008 kikianza na wanachama wachache, na sasa idadi yao imefikia 150.
No comments:
Post a Comment