Habari za Punde

ZANZIBAR YAGOMA KULIPA SH40 BILIONI ZA TANESCO

Salma Said, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekataa kulipa deni la umeme la Sh 40 bilioni kwa TANESCO baada ya kupandishiwa kiwango.Waziri wa Ardhi, Maji, Makazi na Nishati wa Zanzibar , Ali Juma Shamuhuma alisema baada ya kiwango kuongezeka, serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatakiwa kulipa kwa asilimia 168 badala ya asilimia 21 kwa uniti.

Shamhuna alikuwa akichangia katika majumuisho ya mjadala juu ya ripoti ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo Shamuhuna alisema, “hatukubali kulipa deni la Sh 40 bilioni kwa kiwango cha asilimia 168 asilani.”

Tanesco ilipandisha viwango vya malipo kwa wateja wake tangu mwaka jana kwa asilimia 21, kwa upande wa Tanzania bara ambapo kwa Zanzibar shirika hilo la umeme limepandishwa kwa asilimia 168 na kusababisha malalamiko makubwakutoka kwa wateja.Shamhuna alisema kuendelea kwa Tanesco kudai deni hilo kunakwenda kinyume na agizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba pande zote mbili za Muungano zilipe viwango sawa vya asilimia 21.

Waziri huyo ambaye alikuwa akichangia na kupigiwa makofi na wajumbe wengine alisema ili kuepukana na utegemezi wa umeme kutoka Tanesco ambao unaigharimu SMZ fedha nyingi, serikali umeanza kuchukua hatua za kuzungumza na wawekezaji wazoefu ili kuzalisha umeme kutokana na jua na gesi utakaojitegemea.

Shamhuna aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba mradi kama huu umefanikiwa Dubai na Malaysia unaweza kuzalisha kati ya Megawati 50 na 100 ambao unatosheleza mahitaji ya sasa ya Zanzibar ya Megawati 50.

Hata hivyo, akizungumzia kuhusu madai ya baadhi ya Wajumbe wa baraza la Wawakilishi wanaotaka Zanzibar izalishe umeme kwa kutumia mawimbi ya bahari, Shamhuna alisema utafiti unaonyesha kuwa ni mradi mkubwa wenye gharama kubwa na pia haujafanikiwa katika nchi nyingi duniani.

Wakichangia mjadala huo wajumbe wengine wa baraza hilo wamesema suala hilo linahitaji kuangalia vyema na serikali ya muungano kwani haiwezekani serikali hiyo kukaa kimya na baadhi yao kutaka fedha hizo kutolipwa kwani haitowezekana.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Angalia chini baadhi ya maoni

Hapa inaonesha kuwepo umeme wa Tanesco Zanzibar sio kwaajili ya udugu na muungano uliopo, lakini kwaajili ya biashara ambayo itaipatia Bara faida maradufu. Kutokana na hayo, inaonesha wazi kuwa Tanesco inaichukulia Zanzibar ni nchi ya kigeni kama zilivyo nchi nyenginezo. Ama kuhusu petroli ya Zanzibar, upo udugu kwa sababu ni petroli hiyo ni mali ya muungano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.