Habari za Punde

WATOA HUDUMA ZZA MAABARA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Na Ameir Khalid

NAIBU Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi, amewaomba wataalamu wa huduma za maabara Zanzibar
(ZAMELSO), kuzidisha bidii na ubunifu katika kutekeleza majukumu ya uchuguzi wa maradhi mbalimbali, ili tiba sahihi ya maradhi iweze kupatikana.


Alisema wataalamu hao wana jukumu kubwa kwa jamii kwani ili mgonjwa aweze kujulikana maradhi yake, jambo la kwanza ni kupimwa na wao ndio wanaohusika na kazi hiyo, hivyo ni lazima wafanye kazi kwa juhudi zao zote.

Naibu Waziri huyo alitoa kauli hiyo alipofungua mkutano mkuu wa jumuiya ya wataalamu wa maabara Zanzibar (ZAMELSO), Skuli ya Haile Sellassie.

''Daktari mfamasia na muuguzi hawawezi kutoa huduma ya matibabu na dawa  iliyonzuri, kazi kubwa na muhimu inaanza kwenu wachunguzi maana nyinyi ndio mnaosema tatizo alilonalo mgonjwa''alisema.

Alisema ni lengo la serikali kutoa huduma za afya, lakini pia ni jambo la kupongezwa kuona kuwa Zanzibar, zipo taasisi zisizo za serikali ambazo zinatoa huduma ya maabara, yenye malengo ya kuboresha huduma za uchuguzi wa maradhi, yanayowasumbua wananchi na kupelekea tiba sahihi na iliyo bora kwa wakati.

Hivyo aliwaomba wataalamu hao watilie mkazo zaidi katika kutoa huduma kwa jamii, bila ya kubagua pia wahakikishe huduma za wanajumuiya zinafika takriban vituo vyote vya afya, vikiwemo vya serikali na sekta  binafsi pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama.

Katika hatua nyingine wanajumuiya hao wa ZAMELSO wamejadili na kuifanyia marekebisho katiba kwa lengo la kuhakikisha upungufu wote uliokuwemo unarekebishwa.

Mapema wajumbe wa jumuiya walipokea na kujadili taarifa ya utendaji wa jumuiya kuanzia mwaka 2009 hadi 2010, ikiwemo ripoti ya kamati tendaji na ripoti ya matumizi ya  fedha za jumuiya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.