Habari za Punde

NAHODHA, VIGOGO WA MELI ILIYOZAMA KORTINI

Talib Ussi, Zanzibar

WATU wanne akiwamo nahodha wa meli Mv Spice Islanders na msaidizi wake, wamefikishwa Mahakama Kuu ya Zanzibar shtaka la kufanya uzembe na kusababisha vifo vya watu 203.


Waliofikishwa mahakamani jana ni Saidi Abdala Kinyanyite (58) mkazi wa Mbagala Dar es Salaam ambaye hakuwepo mahakamani jana na Abdalla Mohd Ali (30) mkazi wa Bububu Zanzibar, wanashtakiwa chini ya kifungu namba 236 cha Sheria ya Zanzibar namba 6 ya mwaka 2004.

Washtakiwa wengine ni Ofisa Usalama wa Bandari na Mdhibiti Mkuu wa idadi ya abiria na mizigo katika meli, Simai Nyange Simai (27) mkazi wa Mkele Zanzibar na Ofisa Mkuu na Mwanahisa wa Meli Spice Islander, Yussuf Suleiman Jussa (47), mkazi wa Kikwajuni.

Akisoma mashtaki ya kesi hiyo Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Geoge Kazi, alidai kuwa, washitakiwa hao siku ya Ijumaa iliyopita waliiruhusu meli ya Mv Spice kupakia mizigo na idadi kubwa ya watu na mizigo kinyume na kiwango walichowekewa kisheria.

Wakili wa Utetezi, Hamidi Mbwezeleni aliiomba mahakama iwape wateja wake dhamana kwani hiyo ni haki yao kikatiba na hasa kwa kuwa kesi hiyo haijatolewa hukumu.

“Kuwaweka ndani ni sawa na kuwahukumu wakati kesi haijafika mwisho,” alisema Mbwezeleni.

Hata hivyo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Ramadhani Nasibu, alipinga ombi hilo kwa kile alichoeleza kuwa dhamana ni kwa usalama wa washtakiwa wenyewe kwani joto la wananchi waliopotelewa na jamaa zao katika ajali hiyo, bado halijashuka.

Mwendesha mashitaka huyo pia alisema kuwa, wanazuia dhamana kwa sababu upelelezi bado unaendelea na kuna uwezekano wa watuhumiwa hao kupatikana na makosa mengine zaidi hayo ambayo yatasababisha adhabu kali zaidi.

Jana washatakiwa hao kwa pamoja, hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani kutokana na mahakama ya Mrajisi kutokuwa na mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Akitoa uamuzi wake, Mrajisi huyo wa Mahakama alisema hatakiwi kukurupuka kuwapa dhamana washtakiwa hao kutokana na uzito wa kesi yenyewe. Akaamuru watuhumiwa wote warudi rumande hadi Septemba 19, mwaka huu.

“Sitakiwi kukurupuka kutoa dhamana naamuru washtakiwa wapelekwe rumande hadi Jumatatu,” alisema George.

Serikali yasitisha utafutaji maiti

Katika hatua nyingine Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza kusitishwa rasmi kwa zoezi la utafutaji wa miili ya watu walionasa kwenye vyumba vya meli ya MV Spice Islander iliyozama eneo la Nungwi Kaskazini mwa Kisiwa cha Unguja, Zanzibar kutokana na ugumu wa kazi hiyo.

Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, alisema kusitishwa kwa zoezi hilo kunatokana na kushindwa kwa wazamiaji wa kimataifa kutoka nchini Afrika ya Kusini kuifikia meli hiyo kutokana na kina kirefu kilichopo eneo la ajali pamoja na hali mbaya ya hewa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, ndiye aliyetangaza uamuzi huo juzi na kueleza kuwa ingawa Serikali ilikuwa na nia ya kuitoa mili yote kwenye meli hiyo, imeonekana kazi ni ngumu mno.

Balozi Idd aliwaomba Watanzania kukubali kuwa ndugu zao waliopoteza maisha na miili yao kushindikana kupatikana ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Balozi Iddi alisema kila mmoja hana budi kumshukuru Mungu na kukubaliana na hali hiyo kwa vile hata kama Serikali ingekuwa na nia ya kuendelea na zoezi hilo, lingechukua muda mrefu na mwisho wa siku, huenda lisingezaa matunda.

"Tangu kuzama kwa meli ya Spice Islander hadi leo, ni muda mrefu kiasi ambacho hata kama miili ingetolewa, isingekuwa rahisi kutambulika kutokana na kuharibika vibaya," alisema Balozi Iddi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.