Adai viongozi wa chama wana viburi
Na Kunze Mswanyama, Dar
SIKU moja baada ya kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la CUF, Hamad Rashid Mohammed amesema hatambui maamuzi yaliyochukuliwa ya kufukuzwa ndani ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Hamad Rashid ambaye ni Mbunge wa Wawi, alisema hakubaliani na uamuzi wa kufukuzwa kutokana na mkutano wa baraza hilo kuipinda amri ya Mahakama Kuu.
Alisema Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa hati ya kusitishwa kufanyika kwa mkutano huo lakini kutokana na kiburi cha viongozi waliokuwa akisimamia mkutano huo katika ukumbi wa hoteli ya Mazson walipinga na
kuendelea na mkutano.
Hamad Rashid alisema kwa mtazamo wake hakuna kiongozi wa ngazi yeyote ambaye ana uwezo wa kudharau amri ya mahakama ambayo ni mhimili watatu wa dola.
“Kama kiongozi anaidharau katiba ya nchi hafai kuwa kiongozi, kwani katiba ndiyo inayoeleza uwezo wa mahakama kama chombo cha chenye uwezo wa kuamua juu ya matatizo, lakini wao wameidharau, wanaomba kuongoza nchi hivi wakipata urais si ndiyo nchi itakufa kabisa”, Rashid alishusha kijembe.
Akijibu juu ya hatima yake kisiasa, Rashid alisema kuwa anatazamia kuanzisha chama chake hapo baadae, lakini kwanza anasubiri apate ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya vyama vya siasa.
Katika hatua nyengine baadhi ya wafuasi wa CUF wamerudisha kadi za chama hicho kwa kile wanachodai kutoridhika na maamuzi ya Baraza kuu ya kumtimua Hamad na wenziwe kwa tuhuma za uasi na kula njama za
kukihujumu chama.
Kwenye ukumbi wa hoteli ya Cristal Palace hoteli, waandishi walishuhudia rundo la kadi zilizorejeshwa kutoka kwa wanachama kutoa wilaya mbali mbali jiji Dar es Salaam, huku wanachama wa wilaya ya
Temeke wakirejesha kadi zipatazo 600.
Wanachama mkoani Tanga wanapanga kurejesha kadi hizo, huku Mwanza wakiandaa kufanya maandamano makubwa ya kupinga kutimuliwa kwa Hamad Rashida na wenziwe.
Mgogoro ndani ya chama hicho ulianza baada ya Rashid kutangaza nia ya kuwania nafasi ya Katibu Mkuu katika uchaguzi ujao ndani ya chama hicho jambo lililoushtua uongozi wa juu wa chama hicho na kumuita ni
msalaiti.
Katika kikao cha kilichofanyika katika ukumbi wa Mazson hoteli mbali ya Hamad na wenziwe watatu kutimuliwa, wapo pia waliovuliwa madaraka na wengine kupewa onyo kali.
No comments:
Post a Comment